Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itazirejesha fedha za ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Msalala zilizorudishwa na mfumo baada ya mwaka wa fedha 2019/2020 kuisha?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa ajili ya majibu ya Naibu Waziri. Maswali mawili ya nyongeza; nini commitment ya Serikali kuhusu tabia ya kuzichelewesha fedha na baada ya muda mfupi kuzirejesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili…

SPIKA: Rudia la kwanza.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Nini commitment ya Serikali kuzichelewesha fedha kuzipeleka Halmashauri na baada ya muda mfupi kuzirejesha?

SPIKA: Swali lako halisomeki, la pili na la mwisho.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Je, halmashauri itakuwa…

SPIKA: Aah! Umechelewesha unarejeshaje tena ulichokichelewesha.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: mfumo unazichukua zile fedha…

SPIKA: Naam.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Kwamba inachelewesha kutuma fedha mpaka mwezi wa tano au wa nne lakini baada ya muda mfupi tu mfumo unazirejesha kwenda Hazina kabla zile fedha hazijatumika.

Nini commitment ya Serikali… (Makofi)

SPIKA: Rudia mara ya mwisho.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Swali la mwisho je Halmashauri…

SPIKA: Hilohilo hujaeleweka

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Sijaeleweka, nasema hivi…

SPIKA: Unajua anatoka Shinyanga ni Msukuma huyu sasa inakuwa tabu kidogo.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Nini commitment ya Serikali kuhusu suala la kuchelewesha fedha kuzituma katika halmashauri husika na baada ya muda mfupi kuzirejesha kupitia huo mfumo?

SPIKA: Yaani anachosema hela inacheleweshwa kupelekwa kwenye halmashauri hadi kwenye mwezi wa nne/ tano si bajeti inaisha mwezi wa sita halafu wakishazituma kwenye halmashauri mwezi ule wa nne/tano baada ya wiki mbili/tatu wanazichukua tena fedha zilezile ndicho anachojaribu kukieleza. (Makofi)

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa elaboration.

SPIKA: La mwisho.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, la mwisho; je, halmashauri itakuwa inatenda kosa ikizikatalia zile fedha zisirejeshwe kwenye mfumo?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 inaeleza vizuri utaratibu wa fedha zinazopelekwa kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zimepangiwa majukumu mahususi lakini hazitatumika mpaka tarehe 30 Juni ya mwaka husika wa fedha.

Utaratibu uliolekezwa na sheria ni kwamba Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wakishaona fedha zimeingia kwa kuchelewa na kwa mazingira halisi hawawezi kuzitekelezea majukumu yake by tarehe 30 Juni ya mwaka husika wanatakiwa kuandika barua kwa Katibu Mkuu Hazina kupitia Katibu Mkuu TAMISEMI kuomba maombi maalum na kutoa sababu za msingi kwamba fedha zile hazitaweza kutumika kwa tarehe husika na hivyo wapewe kibali maalum cha kutumia fedha zile ndani ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha unaofuata kwa maana ya Julai, Agosti na Septemba ya mwaka wa fedha unaofuata.

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo, Wakurugenzi wengi wamekuwa hawaitekelezi ipasavyo sheria hiyo na nichukue nafasi hii kutoa wito na maelekezo kwa Wakurugenzi wa halmashauri kwanza kuhakikisha wanaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mara wanapopokea fedha lakini pili kutekeleza sheria hiyo kwa kuomba kibali maalum cha matumizi ya fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, pili; mifumo ambayo kimsingi inatumika katika kupeleka hizi fedha na kutumia katika mazingira hayo zina changamoto zake lakini Serikali inaendelea kuboresha kuhakikisha karibu na mwisho wa mwaka mifumo hii inafanya kazi na kuwezesha miradi ya maendeleo kutekelezwa.