Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASHA A. JUMA aliuliza:- Kumekuwa na muingiliano wa wananchi kuishi karibu, ndani au pembezoni mwa maeneo ya Kambi za Jeshi kama ilivyo kwenye Kambi ya Chukwani. (a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenganisha maeneo hayo na makazi ya wananchi kwa kuweka mipaka madhubuti? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kushughulikia suala hili mapema ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea baina ya Jeshi na wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. ASHA A JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa mwingiliano baina ya wananchi na kambi ni mkubwa, sasa pamoja na hatua za miti na kuta, ni kwa kiasi gani au ni tahadhari gani ya ziada zilizochukuliwa kukabili matokeo ambayo hayatarajiwi ya bahati mbaya kama yale yaliyotokea Gongolamboto na Mbagala? Na nataka nithibitishiwe hapa kwamba wahanga wote wa Gongolamboto na Mbagala kama walishapata fidia?
Swali la pili, ni kwamba Jeshi linapopanua sehemu zake hizo huwa linatoa fidia. Je, katika suala hili limejipanga kiasi gani katika mpango wa kulipa fidia kwa wananchi ambao inawahamisha? Ahsante.

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (Kn.y WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Serikali kwa swali lake la kwanza ni kwamba mpaka hivi tunavyoongea hapa tayari ndani ya Jeshi kuna mikakati ya kujenga maghala mapya na kwa kiasi kikubwa maghala mapya ya kuhifadhia ilaha yamekwisha kamilika kwenye vikosi mbalimbali, kambi mbalimbali. Japakuwa sitovitaja ni vikosi gani kwa sababu za kiusalama, lakini tayari mabomu na vifaa vyote vya milipuko vya Jeshi vimekwishahamishwa kwenye kambi ambazo zipo karibu zaidi na wananchi na kuwekwa kwenye maghala hayo mapya ili kuondoa uwezekano wa matatizo kama yale yaliyojitokeza pale Mbagala na kule Gongolamboto.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa fidia tayari naamini utakuwa ulishaanza na pengine ulishamalizika sina uhakika sana na hilo, naomba nisiseme lolote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili, kuhusiana na wananchi kupatiwa fidia kwenye maeneo ambayo Jeshi linaonekana limevamia. Kiukweli ni kinyume chake. Jeshi limekuwepo katika maeneo haya ya makambi kwa kiasi kikubwa lakini wananchi ndiyo wamekuwa wakivamia maeneo ya majeshi. Lakini kwa kuwa Jeshi hili ni la wananchi na ni rafiki kwa wananchi, japokuwa wananchi wanavamia Jeshi mara kadhaa limekuwa hata likilazimika kuhamisha mipaka yake kutoka kule waliko wananchi na kuingiza ndani zaidi kwenye maeneo yake. Pamoja na kwamba wanayahitaji hayo maeneo lakini Jeshi kwa sababu ni la wananchi na ni rafiki kwa wananchi limekuwa likifanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niwasihi wananchi wote ambao wapo karibu na maeneo ya Jeshi wasiendelee kuwa na tabia ya kuvamia maeneo ya majeshi na tayari sasa hivi Serikali imeshaanza kubaini mipaka yote ya kambi za majeshi na kupanda miti kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi na kwenye kambi hizi ndogo ndogo kuweka fence aidha ya wavu ya ukuta. Ninaamini tunapoelekea matatizo kama haya ya mwingiliano baina ya wananchi na Jeshi hayatojitokeza.