Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Bupe Nelson Mwakang'ata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Mradi mkubwa wa Maji wa Kabwe katika Wilaya ya Nkasi utakamilika?

Supplementary Question 1

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwanza kabisa naishukuru Serikali imeweza kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwenye mradi huu. Mradi huu ulifanya kazi miezi mitatu tu na watu wakaihujumu ile miundombinu kwa kuiba vifaa kama solar, betri na pampu. Sasa swali langu linakuja, ni lini sasa Serikali itarudisha vifaa hivi ili wananchi waweze kuendelea kupata maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wezi wapo wanajulikana kabisa kwenye Kata ile, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwachukulia hatua kazi za kinidhamu? Ahsante.

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake namba moja lini vifaa vile vitarudishiwa pale kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi na kadiri ambavyo tumekuwa tukiongea naye kuhusu suala hili na nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa mfuatiliaji mzuri. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili hatutazingatia zaidi kwenye vile vifaa vya solar, tutazingatia kuleta umeme kwa kupitia REA ili tuwe na umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na wale wezi kuchukuliwa hatua, kwanza niombe ushirikiano Zaidi, tuendelee kuwasiliana, hawa wezi Mbunge akiwa kama mwakilishi wa akinamama wa eneo lile, aende akaripoti polisi, lakini tumekuwa tukimsikia mara nyingi Mheshimiwa Waziri wetu kwamba mwisho wa kuchezea miradi ya maji ni sasa. Kama una mambo ya kutaka kuchezea, kachezee kitambi chako. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha kwamba miradi ya maji mwisho kuchezewa. (Makofi)

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:- Je, ni lini Mradi mkubwa wa Maji wa Kabwe katika Wilaya ya Nkasi utakamilika?

Supplementary Question 2

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nishukuru majibu ya Naibu Waziri. Waziri Mheshimiwa Mbarawa akiwa Waziri wa Maji alipofika kwenye mradi huu aligundua shida ni mfumo ambao ni umeme wa kutumia jua na kwa sababu huo mradi wa REA bado haujaanza kufanya kazi Kata ya Kabwe, ni lini watashirikiana na Wizara ya Nishati ili wananchi wa Kijiji cha Odachi, Kabwe Camp pamoja na Kabwe Asilia waweze kupata maji? (Makofi)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri wangu kwa namna nzuri anavyojibu maswali. Sisi Mawaziri viongozi wetu wametuelekeza kufanya kazi kwa pamoja na tumeshafanya mawasiliano na Mheshimiwa Waziri wa Nishati kuainisha maeneo yote yenye miradi yenye mfumo wa jua kuhakikisha kwamba tunafanya mageuzi kuweka mfumo wa REA kwa maana ya nishati ya umeme ili kuhakikisha kwamba tunapunguza gharama ya uendeshaji ili wananchi waweze kupata huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Aida hili jambo tumeshakaa na tumeshaainisha kwa hiyo wenzetu wa nishati watatupa nguvu kuhakikisha maeneo yote yenye solar tunafanya mabadiliko kuhakikisha kwamba tunaweka nishati ya umeme. Ahsante sana.