Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Makanya kwenda kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same?

Supplementary Question 1

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni ukweli usiopingika kwamba ni barabara ambayo haipitiki kipindi chote cha mvua. Ni barabara ambayo inaleta manufaa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa madini ya jasi ya Makanya yanalisha viwanda vya Tanga Cement, Twiga Cement, Moshi Cement, Doria Arusha na nchi za Rwanda na Burundi na kuiingizia Serikali mapato. Serikali haioni haja ya kuiboresha barabara kwa kuitengea fedha ili iweze kufanya kazi muda wote na kuongeza mapato ya Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, katika machimbo haya wako wanawake ambao wamewekeza kule ambao wamepata fursa ya kuendesha biashara ya mama lishe na biashara ndogondogo. Je, Serikali haioni kwamba kwa kusimama kwa machimbo haya kutokana na barabara korofi wanawake hawa wanadhoofika kiuchumi? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza maswali mawili ya msingi kabisa ambayo yana nia njema ya kuwasaidia wanawake wote wa Same mpaka Mkoa mzima wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza la msingi ambalo ameuliza hapa, amesema barabara hii haipitiki na ameomba Serikali tutenge fedha. Kwa kuwa maombi haya yametoka kwa mtu ambaye ameshakuwa kiongozi ndani ya chama na ni maombi muhimu sana,
nimwambie tu kwamba tutatuma wataalam wetu wa Ofisi ya Rais, TARURA, waende katika eneo hilo wakafanye tathmini ya kina na kuileta ofisini ili tuone namna ambavyo tunaweza tukasaidia barabara hii iweze kupitika wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amesema kwamba kusimama kwa machimbo ya jasi kunasababisha uchumi kwa akina mama kuyumba na kuomba watu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kusaidia ili barabara hiyo iweze kujengwa. Kama nilivyojibu katika jibu la msingi kwamba tutahakikisha barabara hiyo inatengenezwa na inapitika kwa wakati wote kuhakikisha tunasaidia akina mama hao wanaoendesha biashara zao maeneo yale lakini vilevile tunawasaidia wananchi wa Same.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Makanya kwenda kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same?

Supplementary Question 2

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Katika majibu ya msingi, Naibu Waziri ametueleza kwamba kwa kipindi kifupi Serikali imewekeza pale takribani shilingi milioni 130 hivi kwa kuweka changarawe na kukarabati. Hata hivyo, kila baada ya ukarabati huo, mvua ikija inazoa changarawe zile na shida inabakia palepale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na shida ambazo mwenye swali alishazizungumzia, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wa kuanza kuweka lami katika kilometa chache chache ili shida hiyo ya kupoteza hela za Serikali iishe? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba tunatuma wataalam wa TARURA pale wakafanye tathmini na baada ya tathmini hiyo watakayotuletea ndiyo tutafanya maamuzi ya kwamba sasa ijengwe hilo lami kama ambavyo nilimjibu mwenye swali la msingi, ama tuweke kiwango cha changarawe. Kitu ambacho nina uhakika nacho ni kwamba Serikali yetu ni makini na inasikia, lengo lake ni kuhakikisha barabara hiyo inapitika kwa wakati wote. Ahadi zetu siyo za uongo, tuko hapa kwa ajili ya kufanya kazi na tutahakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote.

Name

Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Primary Question

MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Makanya kwenda kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same?

Supplementary Question 3

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa akina mama wa Jimbo la Same Magharibi wengi wao nao pia wako katika Machimbo haya ya Jasi na wanachimba jasi kwelikweli. Je, Serikali haioni kwamba ni muhimu hawa akina mama kupata mikopo maalum kwa sababu uchimbaji wa jasi unatumia pesa nyingi? Kama inawezakana, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuwapa mikopo akina mama wote wa Tanzania ambao wanachimba madini? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu swali la msingi lilikuwa linataka tujenge barabara tuwasaidie, lakini miongoni mwa majibu ambayo tulikuwa tumetoa ni pamoja na kuwainua akina mama ambao wanafanya kazi katika machimbo hayo ya jasi.

Mheshimiwa Mbunge wa Same Mashariki amependekeza Serikali itenge fedha kwa ajili ya kupeleka mikopo na sisi sasa hivi katika moja ya sheria ambazo tulipitisha ndani ya Bunge ni kuhakikisha zile asilimia kumi za mikopo kutokana na mapato ya ndani zinakwenda katika hayo makundi ya akina mama, vijana na watu wenye mahitaji maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na nafikiri moja ya kipaumbele ambacho tutakizingatia ni hicho. Ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Silinde kwa majibu mazuri. Vile vile nampongeza Mheshimiwa Mama Anne Kilango, ame-raise humu ndani hoja ya msingi sana ya kutambua makundi maalum na hasa ya wanawake yenye mahitaji maalum ya mikopo kwa ajili ya shughuli za kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mama Anne Kilango, pia niwatangazie na Wabunge wengine wote, kupitia mpango maalum wa Serikali, tayari tumeanzisha mfuko maalum wa SUNVIN; tunauita hivyo kwa ajili ya ku-support shughuli hizi za akina mama na wafanyabiashara wadogo na wa kati ili waweze kuji- transform na kufanya biashara kubwa na hasa za uwekezaji kwenye viwanda, madini na shughuli nyingine zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, mnaweza kuwasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili mpate taarifa ya mfuko huo akina mama na Watanzania wengine waweze kuanza kuutumia. Tayari mfuko huo umeshakuwa na fedha na umeshaanza kutumika kufanya uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali nchini. (Makofi)

Name

Kasalali Emmanuel Mageni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Primary Question

MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Makanya kwenda kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same?

Supplementary Question 4

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa hali ilivyo katika eneo la Makanya huko Same inafanana moja kwa moja na hali ilivyo katika Kata za Mwabomba na Mwandu katika Jimbo la Sumve, ambapo barabara za kutokea Mwabomba kupitia Chamva - Mulula mpaka Manawa hazipitiki katika kipindi chote cha mvua:-

Je, lini sasa Serikali itaamua kuzijenga kwa kiwango barabara hizi ili ziweze kupitika katika mwaka wote ili watu hawa waweze kufanya shughuli zao za maendeleo? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Kasalali Mageni ameainisha maeneo ya Kata kadhaa, kama nne hapa ambazo hazipitiki kabisa. Nami tu niwaagize TARURA Makao Makuu, ninaamini hapa wananisikiliza, wakafanye tathmini kama ambavyo nimeagiza katika eneo la Same ili walete hiyo taarifa. Kwa sababu sasa hivi tunahitaji tathmini za kina ili tuhakikishe hizi barabara tusiwe tunazungumza tu hapa, tunaleta maneno maneno. Tuzungumze kwa data na tuhakikishe kabisa kila barabara, hususan zile ambazo hazipitiki kabisa tunazitengea fedha na kila fedha inayopatikana inajenga ili kuhakikisha barabara zote zinapitika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nilichukue hilo jambo na tayari nimeshaagiza sasa hivi, watafanya tathmini na nitaleta majibu kupitia Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)