Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:- Utaratibu wa watoto kuingia darasa la kwanza ni lazima awe amepitia shule za awali. Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha madarasa ya elimu ya awali?

Supplementary Question 1

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa kuandikisha watoto kuingia darasa la kwanza kunakuwa na sharti la Watoto kwamba ni lazima waje na certificate ya kumaliza elimu ya awali; na changamoto hii imekuwa ni kubwa sana katika maeneo ya pembezoni mwa Mkoa wa Dar es Salaam katika shule kama za Mbande, Majimatitu, Charambe, Nzasa na maeneo mengi ya Mkoa wa Dar es Salaam:-


Je, Serikali inatoa kauli gani sasa kuondoa changamoto hii kwa wananchi au wazazi ambao wanapeleka watoto wao kuwaandikisha darasa la kwanza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa uwiano wa darasa la kwanza utakuta kuna mikondo minne au mitano ya lakini darasa la awali linakuwa moja tu, jambo ambalo ni changamoto kubwa kwa watoto wote ambao wanaanza darasa la kwanza kwenda kujiunga na elimu ya awali katika shule husika:-

Je, Serikali imejipangaje sasa kuweka bajeti ya kutosha katika kuimarisha elimu ya awali katika shule zote za msingi? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali hapa kwamba kumekuwa na sharti la certificate ya Elimu ya Awali; na anataka kufahamu Serikali inatoa kauli gani? Kwanza nieleze tu kabisa kwamba katika ngazi ya awali, Serikali haina utaratibu wa certificate. Hizo ni taratibu ambazo watu wamejitungia huko chini. Mara nyingi sana ni hizo shule za private zaidi ndiyo wamefanya hivyo, lakini huo utaratibu haupo.

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali ni moja tu; certificates zilizopo ni za darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita na kuendelea, lakini kwa shule za awali certificate hakuna. Huo ni utaratibu ambao Serikali haiutambui. Kwa hiyo, hiyo ndiyo kauli ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, uwiano wa wanafunzi, hususan darasa la kwanza na shule ya awali; na kwa sababu hiyo niseme tu kwamba kutokana na umuhimu wa kuongeza wanafunzi katika shule za awali, ndiyo maana sasa hivi katika mipango yote ya Serikali ambayo tunayo, ikiwemo EP4R, Boost, Lens, RISE, miradi yote, tumehakikisha kabisa kwenye kila mradi tunaweka na component ya kujenga madarasa ya shule za awali ili kuhakikisha watoto wetu wanapata madarasa bora na tunaongeza madarasa ili watoto hao waweze kupata mazingira bora ya kujifunzia.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na vile vile nampongeza Mheshimiwa Mariam Kisangi. Nataka tu kuendelea kutoa tamko la kisera; ni marufuku shule kudai certificate ya awali kwa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni kwamba bado hatujafanya vizuri katika kuongeza access ya watoto kuanza elimu ya awali. Kwa hiyo, haileti mantiki kusema kila mtoto ili aanze Darasa la Kwanza awe na certificate ya awali. Tunawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwenda kuweka nguvu za kuboresha watoto wetu hususan wa masikini kupata elimu ya awali, hususan katika maeneo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona niweke hiyo; na wote ambao wanadai certificate ya elimu ya awali wajue kwamba wanatenda kinyume na maelekezo na miongozo ya Serikali.