Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Primary Question

MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y. MHE. KATANI A. KATANI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi wa Kata za Mnyawa, Nanhyanga, Nambahu, Kitama na Nguja ambao wameanza kujenga vituo vya afya kwa nguvu zao wenyewe kwa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo?

Supplementary Question 1

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Jimbo la Tandahimba pamoja na Newala Vijijini lina changamoto ya upatikanji wa vifaatiba pamoja na vitenganishi hali ambayo wakati mwingine inasababisha akinamama wanaojifungua kwenda kutafuta kadi za kliniki mitaani. Je, upi mpango wa dharura wa Serikali wa kunusuru hali hiyo ya upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na vitendanishi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Jimbo la Newala Vijijini lenye Kata 22 lina vituo vitatu tu vya kutolea huduma za afya hali ambayo inaleta changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wake. Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Jimbo la Newala Vijijini ili wananchi wale wapate huduma za afya kama ambavyo inahitajika? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya utoaji huduma za afya katika vituo vya afya kwanza kwa kutenga fedha kwa ajili ya kununua vifaatiba, vitendanishi lakini pia ununuzi wa dawa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha huu tunaoendelea nao Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 26 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba na tayari shilingi bilioni 15 zimekwishanunua vifaatiba na vimekwishapelekwa kwenye vituo vya afya vya awamu ya kwanza na awamu ya pili. Kiasi cha shilingi bilioni 11 kiko katika hatua za manunuzi na mara moja vifaa hivyo vitanunuliwa na kupelekwa kwenye vituo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kituo cha afya katika Jimbo la Newala ni moja ya vituo vya afya vilivyojengwa katika awamu ya tatu na ya nne na hivyo vituo hivi vitakwenda kutengewa fedha za ununuzi wa vifaatiba katika mwaka wa fedha 2021/ 2022. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Maimuna Mtanda kwamba vituo vyake hivi vya afya vitawekewa mpango wa kununuliwa vifaatiba ili viendelee kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na idadi ya vitu vya afya katika kata za Jimbo la Newala Vijijini, ni kweli Serikali inatambua kwamba bado kuna uhitaji mkubwa wa vituo vya afya katika kata za Jimbo la Newala Vijijini na nchini kote kwa ujumla na ndiyo maana katika mwaka wa fedha ujao ambapo Mheshimiwa Waziri atawasilisha Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tunatarajia kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya afya katika kata za Jimbo hili la Newala na nchini kote kwa ujumla. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hili litaendelea kufanyiwa kazi.