Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. NAPE M. NNAUYE K.n.y. MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha gharama za kuhamisha umiliki wa ardhi ambazo siyo rafiki hasa kwa wanyonge na kusababisha wengi kuwa na miliki bubu?

Supplementary Question 1

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa umilikaji halali wa ardhi utaisaidia Serikali katika kukusanya mapato kwa sababu wamiliki halali watalipa kodi vizuri na kwa kuwa kwa uzoefu uliooneshwa kutokana na shida ya uhamishaji wa umiliki unaonesha kwamba wananchi wa kawaida wanashindwa kumudu gharama. Je, Serikali iko tayari ikiwezekana kufuta kabisa gharama za kuhamisha umiliki ili wamiliki waweze kumiliki na kulipa kodi kwa Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa maombi ya wananchi wa Mtama walifuta umiliki wa shamba la Maumbika lililoko Jimboni Mtama na kulikabidhi kwetu, lakini tukiwa katika utaratibu wa kuligawa kwa wananchi, Serikali hiyo hiyo ili-reverse uamuzi wake. Je, Serikali iko tayari sasa kutumilikisha shamba hili ili wananchi waweze kulitumia kwa sababu limetelekezwa kwa muda mrefu na mmiliki wa shamba hili? (Makofi)

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nape, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka tu nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii ni sikivu na kila mara wananchi wanapotoa kilio chao, Serikali hukaa na kuanza kuangalia upya kuweza kuona ni jinsi gani tunaweza kuwasaidia. Kwa hiyo katika suala zima la kusema kwamba pengine gharama ya uhamishaji miliki iweze kufutwa ili watu waweze kumiliki wengi bila tatizo lolote, naomba niseme tu Serikali hii inaendeshwa kwa kodi za wananchi. Sasa ukishaanza kuzifuta kodi ambazo pengine ni ndogo na ni token ukiziangalia, mwisho wa siku utakuta Serikali haina njia nyingine yoyote ya kupata mapato na kujikuta kwamba tunakwama. Tunachofanya kama Serikali ni kuendelea kupunguza zile kodi ambazo pengine zina kelele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nikizungumzia suala la muuliza swali ambaye aliuliza swali la msingi, Mheshimiwa Stella Manyanya kwenye eneo lake hata zile tozo wanazotoza katika masuala mazima ya ardhi ziko chini sana. Ukiangalia kwenye makazi walikuwa wanatozwa shilingi 15 lakini sasa hivi wanatozwa shilingi 11 ambazo ni kidogo sana. Kwenye maeneo ya biashara ilikuwa shilingi 30, sasa hivi wanatozwa shilingi 21, hata shilingi 100 haijafika. Ni ndogo ndogo ambazo wananchi wakiweza kulipa kwa hiari ni pesa ambazo unaweza ukazikusanya na zikafanya kazi kubwa katika Taifa hili. Kwa sababu wazo limetolewa, naomba tulipokee na sitaweza kulitolea maamuzi sasa hivi kwa sababu ni lazima mchakato uweze kupita.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameongelea suala la shamba la Maumbika kwamba Serikali ilifuta umiliki wake kwa kushindwa kulimiliki halafu baadaye pengine maamuzi yakabadilika. Naomba niseme kwamba, wakati mwingine tunapotoa ilani kwa ajili ya kubatilisha milki za watu, tunaangalia hatua iliyofikiwa lakini halmashauri husika ndiyo inayoleta notice au maombi yake kwa Waziri kuomba shamba lile lifutwe kwa sababu wameshindwa kutimiza masharti lakini wakati huo wanakuwa wamempa notice ya siku 90 ili aweze pengine kujitetea kwamba kwa nini hakuweza kumudu au kufuata masharti yale yaliyowekwa. Kwa hiyo utetezi unapokuwa wakati mwingine una uhalali na mantiki ndani yake, Serikali pia huwa inabadili mtazamo wake na kuweza kumrudishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa suala hili la Maumbika ambalo amelizungumza lazima kuna kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika hilo kwa sababu sikuweza kuliangalia kwa undani wake kuweza kujua ndiyo amelitoa sasa hivi. Basi kama lina maelezo ya ziada zaidi ya hizi taratibu za kisheria, niko tayari kumjibu baadaye. (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana na ya uhakika ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka tu kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba nchi hii kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Na. 5 Ardhi ya Vijiji na Na. 4 Ardhi ya Jumla tunatoa hati mbili. Kuna hati ambayo ndiyo hiyo inayosababisha wanyonge wananchi wanamiliki, tuna hati ya kimila ambayo inatolewa kwa mujibu wa sheria ambayo zaidi ya asilimia 90 ya hao wanyonge wa nchi hii wanapewa hati za kimila na ndizo zilizo nyingi kuliko hizi hati za mjini. Hawatozwi pesa ya kuanzia wala ada ya kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka niwaambie kwamba Serikali kupitia Bunge hili mlitunga sheria nzuri sana inayowatambua wanyonge. Wanyonge wote wanaomilikishwa zile ardhi wanazozitumia kwa shughuli zao za uzalishaji wa kila siku hawatozwi lolote, hawana kodi ya uhamishaji wala hawana kodi ile la land rent ya kila mwaka na hawana ukomo. Ana miliki leo, hana miaka 33 wala miaka 99 kama hati za mjini. Kwa hiyo suala la wananchi maskini wametambuliwa kwa mujibu wa sheria na waendelee. Hivi sasa Bunge lako halijawahi kutunga tozo yoyote kwa wananchi maskini wanaomiliki ardhi kwa mujibu wa sheria hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili la Maumbika, nalijua vizuri. Tulikuwa na makusudi ya kufuta na ni kweli yule mwekezaji ametelekeza lile shamba. Nataka uwaambie wananchi wa Jimbo lako la Mtama, leo nakupa ahadi, nitakapokuwa naosma bajeti hapa, nitakupa barua nataka lile shamba limilikiwe na Halmashauri ya Wilaya ya Mtama ili wananchi wa pale waliendeleze iwe sehemu ya mapato yao. Walime korosho kwa sababu lile shamba ni la korosho, mmiliki alilitelekeza siku nyingi, tuko kwenye hatua za mwisho za kuliondoa, lakini kwa sasa ningeomba watu wa halmashauri waendelee kuliangalia angalia, kama kuna korosho humo waanze kuokotaokota. Barua kamili ya umiliki wa shamba lile kurudi halmashauri nitaitoa hapa wakati nitakapokuwa nawasilisha bajeti yangu. (Makofi)

Name

Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAPE M. NNAUYE K.n.y. MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha gharama za kuhamisha umiliki wa ardhi ambazo siyo rafiki hasa kwa wanyonge na kusababisha wengi kuwa na miliki bubu?

Supplementary Question 2

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza. Naomba kuuliza swali moja; Serikali imeweka mfumo wa kidigitali wa kulipa kodi za ardhi, lakini mfumo huo haumruhusu mwananchi kupata control number moja kwa moja, ni mpaka afike kwenye ofisi za ardhi ili kuhamasisha ulipaji kodi kwa haraka na kumwepushia mwananchi kulipa faini zisizo za lazima, je, Serikali haioni haja ya kuboresha mfumo huu ili kumwezesha mwananchi kulijua deni lake moja kwa moja kama wanavyofanya Wizara ya Maji? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanaisha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna changamoto katika suala zima la kuweza kupata zile bill kupitia mtandao, lakini bado kama Wizara tulirahisisha kwa kutumia simu zetu ukipiga *152*00# unafuata maelekezo kama ambavyo tunafanya katika masuala ya M-Pesa na mambo mengine. Suala la msingi unalotakiwa kujua wakati unatafuta kujua bill yako unatakiwa uwe unajua plot number yako ya kiwanja au namba ya hati yako kwa sababu itakuuliza na wakati huo itakuuliza kama kiwanja chako kiko Dar es Salaam au kiko mikoani. Kwa Dar es Salaam unaweka namba moja (1) lakini kwa mikoani unaweka namba mbili (2) halafu unafuata maelekezo. Kwa hiyo kuna wakati mwingine mitandao inasumbua, kweli inakuwa ni shida lakini ukiweza kupata mahali ambapo mfumo umekaa vizuri, bado unaweza ukapata bill yako, unaweza ukalipa kodi yako kwa kutumia simu yako hiyo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kama Wizara pia tunajaribu kuboresha mifumo kwa sababu kuna wakati mwingine unadaiwa 500,000 una 300,000 unataka kulipa. Ule mfumo mara nyingi hauruhusu kulipa part payment, inabidi uwasiliane na Afisa Ardhi ili aweze kukupa. Sasa hivi wataalam wetu wanafanyia kazi hiyo ili uweze kulipa hata kama una sehemu ndogo ya kuweza kulipa basi utalipa part payment na nyingine utakuja kumalizia na mfumo utapokea na Wizara ndiyo kazi inayoifanya sasa hivi. (Makofi)