Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Stendi ya Mabasi Makete Mjini?

Supplementary Question 1

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini nilikuwa napenda kumuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Makete ya mwaka 2014 na Makete ya sasa ni ya tofauti sana. Kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imejengwa lami ambayo imefika hadi Makete, na kwa hiyo mabasi kutoka Dar es salaam na mikoa mingine tayari yameshaanza kuingia Makete.

Je, Serikali ipo tayari kutupatia fedha kutoka kwenye mpango wa miradi ya kimkakati ili Makete ipate kituo cha mabasi kizuri ambacho kinaendana na uhitaji mkubwa wa sasa ambao tunao?

Mheshimiwa Spika, jambo la pili; nakuomba Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya Bunge hili kama utakuwa tayari twende Makete kwa ajili ya kuangalia ukubwa wa uhitaji wa kituo cha mabasi pale ndani ya Wilaya ya Makete. Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Makete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Festo Richard Sanga kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kuwatetea wananchi wa Jimbo la Makete katika miradi mbalimbali ya kiuchumi pamoja na ya kijamii.

Mheshimiwa Spika, pili, nimhakikishie kwamba Serikali inatambua kwamba baada ya utekelezaji mzuri wa Ilani na barabara ya lami kutoka Njombe kwenda Makete, ambayo pia itatoka Makete kwenda Mbeya Mji wa Makete utafunguka na una kila sababu ya kupata stendi ya kisasa ya mabasi. Ndiyo maana katika katika jibu la msingi, na ninaomba niendelee kusisitiza, kwamba tunawashauri Halmashauri ya Makete, waandae andiko la kimkakati la ujenzi wa stendi ya mabasi ya kisasa ambalo litaonesha business plan yake na uwezo wa kulipa fedha zile ili tuweze kutafuta vyanzo vya fedha, iwe Serikalini au kwa wadau mbalimbali, lakini pia na mapato ya ndani ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, tatu; nipo tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili. Naomba tukae ili tupange ratiba yetu tufike pale; pamoja na mambo mengine tuangalie ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi. Ahsante.

Name

Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Stendi ya Mabasi Makete Mjini?

Supplementary Question 2

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa uhitaji wa stendi kuu ya mabasi uliopo kule Makete unafanana kabisa na uhitaji wa Stendi ya Mabasi ya Bukoba Mjini. Ningependa kupata kauli ya Serikali; je, sisi Bukoba Mjini tutapata lini stendi mpya ya mabasi hususan ukizingatia kwamba Wilaya ya Bukoba Mjini ndiyo reception ya Mkoa wetu wa Kagera na inaunganisha Kagera na nchi ambazo tunapakana nazo? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Stendi ya Mabasi ya Mji wa Bukoba ni miongoni mwa stendi ambazo Serikali imeziwekea kipaumbele cha kutosha kwa kuhakikisha kwamba kinatafutiwa fedha; lakini pia nitaangalia kwenye miradi ile ya kimkakati ya TACTIC kama Halmashauri ya Mji wa Bukoba imo ili tuweze kujiridhisha kwamba stendi ile itakuwa sehemu ya ule mradi ambao utakwenda kuhudumiwa.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Lugangira, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Steven Byabato, Naibu Waziri wa Nishati na Mbunge wa Bukoba Mjini kwa kazi kubwa ya kufuatilia stendi hii na mambo mengine; na kwamba nimhakikishie, sisi kama Serikali tutashirikiana nao Waheshimiwa Wabunge wote kutekeleza miradi hiyo. Ahsante. (Makofi)

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Stendi ya Mabasi Makete Mjini?

Supplementary Question 3

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri kabla haujawa Mbunge na hatimaye Naibu Waziri tulikuwa wote Manispaa ya Kinondoni; na unafahamu kwamba tulikuwa tuna mpango wa kujenga stendi Kata mashuhuri ya Kawe yenye wananchi wengi sana. Sasa, sasa hivi umeshakuwa Naibu Waziri upo huko kwenyewe huko. Sasa naomba uniambie, kwa sababu mkakati wa Kinondoni unaujua, ni lini tutajenga Stendi ya Kawe? Kwa sababu tuna eneo la iliyokuwa Wizara ya Mifugo na eneo la Tanganyika Packers. Ni lini tutajenga stendi Kata ya Kawe? (Makofi)

Name

Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Dugange kwa majibu mazuri, lakini nimshukuru Mheshimiwa Halima Mdee kwa swali lake, kwamba lini tutajenga stendi katika Kata ya Kawe.

Mheshimiwa Spika, nimesimama, tulipata maelekezo kutoka kwa Kamati yako ya Bajeti lakini pia Kamati ya Utawala na TAMISEMI kwamba tufanye mapitio ya mwongozo wa kutekeleza miradi ya kimkakati nchini, kwa sababu inavyoonekana mwongozo ule unazipendelea Halmashauri zenye mapato makubwa na kuzifanya Halmashauri zenye mapato madogo kutopata rasilimali fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halafu fedha hizi ni grant, ukipewa hazirudi; kwa hiyo tulijadili, na sisi tumekubaliana na ushauri wa Kamati. Unamuacha Makete, unampa Kawe, Kinondoni ambaye ana mapato ya zaidi ya bilioni 30. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha tunapitia mwongozo ili halafu sasa tuweke vigezo vya jinsi ya ku-finance miradi ya kimkakati ili hata Halmashauri zisizo na fedha na mapato ya kutosha waweze kupata fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa stendi, masoko na vitega uchumi vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Kawe itasubiri kwa kuwa kipaumbele chetu tutaangalia uhitaji wa Halmashauri maskini au zenye mapato madogo Zaidi. Ahsante. (Makofi)