Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Hospitali ya kisasa Mkoani Morogoro?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Naishukuru Serikali kwa kuwa na mpango wa kujenga Hospitali ya kisasa kwenye Mkoa wetu wa Morogoro. Hata hivyo, bado kuna tatizo la umilikishaji na nimeambiwa kuwa karibu watakamilisha umilikishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, Hospitali hiyo ya Rufaa ya Morogoro ambayo tunaipanua mpaka sasa hivi haina kifaa cha CT-Scan na hili swali nilishauliza humu ndani, nikaahidiwa lakini mpaka sasa hivi hatujapata kifaa hicho. Je, kifaa hicho tutapatiwa lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kutokana na Mkoa wa Morogoro kuwa katikati na kupokea majeruhi wengi lakini tuna tatizo la mtambo wa oxygen. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutupatia mtambo wa oxygen ili kupunguza matatizo tuliyonayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imedhamiria kuhakikisha inaboresha huduma za afya za kibingwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwepo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro. Katika mipango yake, Serikali imeweka mipango ya kuhakikisha vifaa tiba kama CT-Scan zinapatikana katika hospitali kubwa za mikoa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali iliahidi na ahadi yake bado ipo pale pale. Kazi inayoendelea sasa ni kutafuta fedha ili tuweze kupata mashine hiyo ya CT- Scan na kuifunga katika Hospitali ile ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ili kuweza kuboresha huduma. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo bado linafanyiwa kazi na Serikali na litakamilika ili tuweze kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na umuhimu wa kuwa na mtambo wa oxygen katika hospitali ile, ni kweli, Mkoa wa Morogoro upo kwenye highway ambapo mara nyingi kunakuwa na matukio ya ajali. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuwa na mitambo ya oxygen ili kuwezesha mkoa kuwa na uhakika wa kupata oxygen pale inapohitajika. Jambo hili pia limechukuliwa na Serikali, linafanyiwa kazi, fedha inatafutwa ili mtambo uweze kuwekwa pale na kuboresha huduma kwa wananchi.

Name

Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Hospitali ya kisasa Mkoani Morogoro?

Supplementary Question 2

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kule kwetu Namtumbo kuna vituo vya afya viwili; Kituo cha Afya cha Mkongo na Kituo cha Afya cha Mputa ambavyo vilijengwa mwanzoni mwa miaka 1980 na hali yake kwa sasa hivi ni mbaya sana.

Kwa kuwa wakati ule vilipojengwa kulikuwa hakuna majengo ya upasuaji, je, Serikali inaweza ikatusaidia kutuletea au kututengea fedha kwa ajili ya kukarabati vituo hivyo vya afya na kujengewa vyumba vya upasuaji?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya utoaji huduma za afya na kwa muktadha huu inajumuisha ujenzi wa vituo vya afya, upanuzi na pia ukarabati vituo vya afya. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Kituo cha Afya cha Mkongo na Mputa ni Vituo vikongwe na vinahitaji kufanyiwa upanuzi na vinahitaji kukarabatiwa na kuongezewa baadhi ya majengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kwamba Serikali inachukua hoja hii na kwenda kuifanyia kazi ili tuweze kuona kadri ya upatikanaji wa fedha, tunatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa vituo hivyo na pia kuongeza majengo; yakiwepo ya upasuaji na majengo mengine ili viweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Name

Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Hospitali ya kisasa Mkoani Morogoro?

Supplementary Question 3

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Serikali kwenye ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, kama alivyokiri Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kweli bado kuna uchakavu mkubwa wa vituo vyetu vya afya.

Napenda kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni upi sasa mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tunamaliza kabisa ukarabati wa vituo vyote vichakavu na vikongwe vikiwemo Vituo vya Afya vya Mombo, Bungu na Magoma katika Wilaya ya Korogwe?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnzava, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imefanya kazi kubwa sana katika ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati na pia imefanya kazi kubwa sana katika kukarabati vituo vya afya ili kuwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi. Ni kweli pia kwamba bado kazi ipo na inahitajika kufanyika zaidi na Serikali inatambua kwamba bado kuna vituo vya afya ambavyo ni chakavu na vinahitaji kukarabatiwa vikiwemo vituo vya afya vilivyopo katika Jimbo la Korogwe Vijijini kwa Mheshimiwa Mnzava.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imetenga shilingi bilioni 11 na imeshaainisha hospitali 43 za Halmashauri kwa ajili ya ukarabati na kuongeza majengo ambayo yanapungua ili yaweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Pia mchakato wa kuandaa na kuainisha vituo vya afya chakavu vikiwemo vya Korogwe Vijijini, unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mnzava kwamba vituo vyake pia vitaingizwa katika orodha hiyo ili kadri ya upatikanaji wa fedha viweze kukarabatiwa na kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Name

Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA Aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Hospitali ya kisasa Mkoani Morogoro?

Supplementary Question 4

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha za kutosha kuweza kukarabati na kujenga wodi ya akina mama katika hospitali ya Wilaya ya Mangaka. Hospitali ile imekwisha, je, Serikali inatuhakikishia vipi upatikanaji wa vifaa tiba katika hospitali ile wakati kazi imeshakamilika? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga bajeti ya kununua vifaa tiba katika hospitali zote mpya za Halmashauri
67. Jumla ya shilingi bilioni 33.5 zimetengwa katika mwaka huu wa fedha na tayari taratibu za mawasiliano kati ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Afya na MSD kuona utaratibu wa kupata vifaa tiba katika hospitali zile mpya unafanyika mapema iwezekanavyo ili vifaa vile viweze kupelekwa katika hospitali zetu mpya za Halmashauri na kuanza kutoa huduma zinazotarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mhata na Waheshimiwa Wabunge kwamba hospitali zetu zote na vituo vya afya zilizojengwa, taratibu za kuhakikisha zinaanza kutoa huduma za afya zinaendelea na Serikali inaendelea kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha, kutenga fedha za kununua vifaa hivyo ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Nanyumbu.