Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. NAPE M. NNAUYE K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI Aliuliza: Serikali ina mpango wa kuunganisha mikoa yote kwa mtandao wa barabara za lami, ikiwemo barabara yenye urefu wa kilometa 223 inayounganisha Mikoa ya Njombe na Morogoro kupitia Mlimba ambayo pia iko katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM):- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa upembuzi yakinifu wa kipande cha Ifakara – Kihansi chenye kilometa 125 umekamilika. Je, Serikali iko tayari kuanza kutenga fedha ya kujenga hiki kipande katika mwaka huu wa fedha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili barabara ya Lutamba- Chiponda-Mnara-Nyengedi inayounganisha Halmashauri ya Mtama na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ambayo pia inaunganisha barabara ya Mkoa ya kwenda Ruangwa lakini pia ya kwenda Masasi kwa maana ya Mkoa wa Mtwara, ni barabara ya muhimu sana kwa uchumi wa eneo hili, lakini hii barabara imekuwa chini ya TARURA kwa muda mrefu na TARURA kwa kweli hawana uwezo wa kuendelea kuijenga. Je, Serikali iko tayari kuipandisha hadhi barabara hii sasa ianze kuhudumiwa na TANROADS?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Nape, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoiuliza ya Mheshimiwa Kunambi ni barabara ambayo inaunganisha Mkoa na Mkoa na kwa kuwa usanifu wa kina umekamilika, tunaamini katika bajeti ijayo Serikali itaanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Nikiri Mheshimiwa Kunambi kila anaposimama imekuwa akiipigia sana kelele barabara hii. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi kwamba katika bajeti tunazoanza kuzitekeleza kwa mwaka ujao naamini itatengewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Nape Mbunge wa Mtama sitazitaja barabara zake zimekuwa ni nyingi Lutamba-Chiponda-Mtama-Lindi na kwamba ni barabara za TARURA, naomba Mheshimiwa Nape nimshauri waweze kupitia kwenye taratibu za kawaida za kupandisha hadhi hizi barabara kutoka TARURA kwenda TANROADS ambapo lazima watakaa na Bodi ya Barabara ya Mkoa halafu itakwenda kwenye Kamati ya Ushauri ya Mkoa na baadaye zinakuja kwenye Wizara kwa ajili ya kuziangalia kama zinakwenda kupandishwa hadhi. Kwa hiyo kama zitakuja kwa utaratibu huo nadhani kuna utaratibu zitafikiriwa na Serikali itaona namna gani ifanye ili kuzipandisha hizo hadhi. Ahsante. (Makofi)