Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND (K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA) aliuliza:- (a) Je, Serikali ipo tayari kuwaeleza Watanzania hususani vijana kuwa hatua gani zimechukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwabaini, kuwachunguza na hatimaye kuwahukumu wale wote waliobainika kujihusisha na mtandao wa biashara za dawa za kulevya? (b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana waliotumbukia kwenye dimbwi la matumizi ya dawa za kulevya?

Supplementary Question 1

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante awali ya yote naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na juhudi zote ambazo zimeshafanyika na zinaendelea kufanyika. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina taasisi zake ambazo zinashughulikia matatizo yao ikiwemo mirembe hapa Dodoma na Lushoto na kituo kilichopo Lushoto. Lakini taasisi hizo zina mapungufu katika rasilimali watu, je, Serikali imejipanga vipi sasa kuwezesha taasisi hizo ili wanapozidiwa na wagonjwa hao waweze kupatiwa matibabu hayo kwa haraka?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili , madawa ya kulevya yana urahibu na pia yanaleta msongo wa mawazo ambayo yanapelekea vijana hawa au wote waliotumia kuwa katika hali ngumu sana ya kimaisha hata pale wanapotoka nje ya vituo ambavyo walikwenda kwa rehab.

Sasa Serikali ina mpango gani kuwezesha Chuo chetu cha Ustawi wa Jamii Tanzania ili waweze kupata wataalam ambao watakuwa wanapita au wanasambazwa katika mikoa yote kwenda kuwashughulikia vijana hawa ambao wameshapata shida hiyo? (Makofi)

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niungane na Watanzania wote lakini vilevile niungane na Waheshimiwa Wabunge wote na hasa Kamati ya UKIMWI na Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya kuwashukuru wadau wote ambao wameshirikiana na Serikali katika kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inafanikiwa kwa kiasi kikubwa, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue hatua nyingine kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa nia yake ya dhati na dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inaondokana na tatizo la dawa za kulevya nchini. Mapambano haya ambayo yameongozwa na mamlaka yamesaidia kwa sasa kwa mujibu wa takwimu na tafiti tulizozifanya mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchi tumeweza kufanikiwa kudhibiti uingiaji wa dawa za kulevya nchini kwa asilimia 95, baada ya kufikia hatua hiyo sasa tunakabiliana na hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyazungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza tunakabiliana na suala zima la harm reduction kuhakikisha tunawarejesha katika hali nzuri waraibu wote ambao walikubwa na matatizo hayo. Yapi ambayo ni mpango wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo tumelifanya Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia mamlaka ni kufungua kituo kikubwa cha tiba hapa Dodoma katika eneo la Itega ili warahibu wote ambao wataonekena wanahitaji matunzo ya ziada kupitia nchi nzima waweze kufanikiwa hapo, lakini kupitia madirisha ya hospitali zetu za rufaa katika maeneo mbalimbali kwenye mikoa, madirisha ambayo yanahudumia wagonjwa wa matatizo ya akili yatatumika pia kutoa tiba ya methadon ili kuwahudumia warahibu wote ambao watapatikana kwenye mikoa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu tumegundua warahibu wakitoka kwenye urahibu wanatakiwa wapatiwe shughuli mbalimbali za kufanya ili wasahau shughuli ile ya utumiaji wa dawa za kulevya, lakini waende katika shughuli ambazo zitawaongezea kipato. Ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu tunayo programu ya kukuza ujuzi, sasa tunataka kuwachukua na warahibu wote waliotengemaa tuwafundishe ujuzi, waweze kujiajiri, waondokane na matumizi ya dawa za kulevya, wawe raia wema na wachangie uchumi na maendeleo ya Taifa lao na maendeleo yao wao wenyewe. Kwa hiyo, nalishukuru sana Bunge na Watanzania wote kwa kazi nzuri ya kupambana na dawa za klulevya nchini. (Makofi)