Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Primary Question

MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:- Serikali imefanya kazikubwa sana ya ukarabati wa Shule ya Sekondari Korogwe lakini haikuunganisha nyumba za Walimu zilizopo Shuleni hapo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzikarabati nyumba hizo?

Supplementary Question 1

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kuishukuru Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikitukimbilia pale shule yetu imekuwa na majanga ya moto zaidi ya mara mbili. Tunaishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili nishukuru kwa majibu mazuri niliyopewa na Waziri.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, katika huu mpango wa pili ambapo watakuwa wametafuta fedha, je, Shule ya Korongwe Girls itapewa kipaumbele cha kwanza hasa ikizingatiwa kwamba pia ina watoto wenye ulemavu ili walimu wale wawe na moyo wa kuendelea kufanya kazi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tunazo shule za kata katika Halmashauri zetu kwa nchi nzima ambapo tulikuwa tumeweka mipango kwa ajili ya ujenzi wa maabara lakini kwa bahati mbaya sana Halmashauri nyingine zimeshindwa kukamilisha mahabara hizo. Je, mtakuwa tayari sasa kuweka mpango wa kukamilisha zile maabara zilizoko kwenye Halmshauri zetu ili watoto waweze kupata elimu iliyo bora kuliko bora elimu?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Mary Chatanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Mary Chatanda maana kwa vipindi tofauti tumefanya ziara jimboni kwake Korogwe na awamu ya mwisho tulienda naye katika shule yetu ya Sekondari Korongwe na kuongea na wanafunzi na kubainisha changamoto mbalimbali. Nafahamu kwamba juzijuzi hapa shule ilipata madhara ya bweni kuungua na ndiyo maana nimetuma wataalamu ili bweni lile tulikarabati haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, katika programu hii ya kukarabati, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Chatanda tutakapoanza awamu hii shule ya Korongwe tutaiweka katika awamu ya kwanza bila kigugumizi chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika mpango wa kuhakikisha tunamalizia maabara, kama mnavyokumbuka kwamba hapa katikati tulitoa zaidi ya shilingi bilioni 32.5 kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunamalizia maboma mbalimbali. Tunajua fika fedha hii haitoshi kwani kuna mabweni mengine hayajakamilika.

Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali hata katika mpango wa bajeti ya mwaka 2019/2020 tutahakikisha katika maeneo mbalimbali tunakamilisha ujenzi wa maabara na vifaa. Juzijuzi tumetumia zaidi ya shilingi bilioni 17 ili tupate vifaa vya maabara vijana waweze kufanya practically katika maeneo ya shule.