Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John Peter Kadutu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Primary Question

MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:- Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) unaendelea kote nchini. Katika Jimbo la Ulyankulu bado umeme haujafika katika maeneo mengi:- (a) Je, ni lini sasa umeme utasambazwa katika Kata za Uyowa, Silambo, Igombe Mkulu, Seleli, Nhwande na Kanoge? (b) Hivi karibuni Wilaya ya Kaliua imesajili Shule za Sekondari tano (5) na Vituo vya Afya pamoja na Sekondari ya Mkondo; je, ni lini sasa umeme utafikishwa katika taasisi hizo?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kabla sijauliza maswali ya nyongeza, nitumie fursa hii kuwashukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kuja kutembelea Jimbo la Ulyankulu na kuona changamoto zetu. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, katika vijiji ambavyo vimeshapitiwa na umeme, kumekuwa na upungufu mkubwa sana wa nguzo kiasi kwamba maeneo mengi hayatapata umeme. Je, Serikali inasema nini kuhusu suala hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, umeme kuupeleka kwenye Mgodi wa Silambo, kuna njia mbili. Je, mkandarasi anaweza kuelekezwa umeme kuelekea katika Mgodi wa Silambo ukapitia eneo la Ikonongo badala ya kupita Uyoa kutoka Kaliua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kadutu. Nami nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Kadutu na Wabunge wote wa Mkoa wa Tabora kwa kazi nzuri zinazoendelea katika majimbo yao, hususani katika kufuatilia Mradi wa REA Awamu ya Tatu unaoendelea. Nawashukuru kwa ushirikiano wao kupitia ziara zetu tunazofanya katika majimbo yao, mara zote tunawakuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika maswali yake ya nyongeza, swali lake la kwanza ameeleza kuhusu vijiji ambavyo vinapatiwa umeme na akasema nguzo ni chache, nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu kupitia swali hili la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Kadutu kwamba kwa kweli hii miradi ya umeme kwa kila kijiji inapokwenda kunakuwa na wigo, kilometa na wateja wa awali lakini kazi ya kuunganisha inaendelea. Ndiyo maana kwa kurahisisha zoezi hilo, tumeielekeza TANESCO na wao wataendelea kusambaza kwa bei ileile ya REA ya Sh.27,000. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge Kadutu kwamba kazi hiyo itaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nimtaarifu tu Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa tisa ya awali ambayo Mradi wa Awamu ya Pili ya Ujazilizi unatarajiwa kuanza hivi karibuni na taratibu za manunuzi zinaendelea na kiasi cha shilingi bilioni 169 zimetengwa na Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kazi ya ujazilizi. Kwa hiyo, maeneo ya vijiji ambapo kuna vitongoji havikufikiwa vitafikiwa kupitia Mradi huu wa Ujazilizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Kadutu ameulizia kama tunaweza tukatoa maelekezo ya kupeleka umeme kwenye Mgodi wa Silambo kupitia njia ya kutoka Ikonongo. Nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa ametoa wazo hilo nilichukue na baada ya kipindi cha maswali na majibu tukutane na tuweze kufanya mawasiliano na TANESCO na REA tuone uwezekano huo ambao pengine hautaathiri kilometa ambazo zimetajwa katika mradi wa kupeleka umeme katika mgodi alioutaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

Name

Felister Aloyce Bura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:- Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) unaendelea kote nchini. Katika Jimbo la Ulyankulu bado umeme haujafika katika maeneo mengi:- (a) Je, ni lini sasa umeme utasambazwa katika Kata za Uyowa, Silambo, Igombe Mkulu, Seleli, Nhwande na Kanoge? (b) Hivi karibuni Wilaya ya Kaliua imesajili Shule za Sekondari tano (5) na Vituo vya Afya pamoja na Sekondari ya Mkondo; je, ni lini sasa umeme utafikishwa katika taasisi hizo?

Supplementary Question 2

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Dodoma ni Jiji ambalo lina vijiji na lina vijiji 34 ambavyo tulikwishapeleka ombi kwa Wizara na Mbunge wa Jimbo hili aliwahi kutembelea maeneo hayo pamoja na Waziri mhusika na tuliomba kupatiwa umeme wa REA. Naomba wananchi wajue ni lini sasa vile vijiji 34 ambavyo tuliviombea umeme wa REA vitapata umeme?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la mama yangu, Mheshimiwa Felister Bura kuhusu vijiji 34 vya Jiji la Dodoma ambavyo vinahitaji umeme wa REA. Kwanza nimpongeze yeye mwenyewe kwa kazi nzuri ya kuwasemea wanawake wa Dodoma lakini pia nimpongeze Mbunge wa Jimbo naye Mheshimiwa Mavunde amekuwa akifuatilia na tumefanya ziara katika Jimbo lake hili la Dodoma Mjini, Mheshimiwa Waziri na mimi mwenyewe tumetembelea Jimbo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu hivi vijiji 34 vipo katika Mpango wa Ujazilizi Awamu ya Pili. Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa tisa na tunakamilisha taratibu za manunuzi na kuanzia kipindi hiki cha mwezi wa Septemba na Oktoba tutakuwa tumeshawapata wakandarasi na kuwakabidhi site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilitaarifu Bunge lako kwa kuwa Dodoma sasa imekuwa ni Jiji na ni Makao Makuu ya Serikali, kwa kweli moja ya mikoa ambayo iko katika kipaumbele cha kusambaza miundombinu ya umeme Mkoa wa Dodoma nao upo. Hata tulivyowaelekeza TANESCO kuendelea kuwaunganisha wananchi kwa bei ya Sh.27,000, Mkoa wa Dodoma nao mpaka sasa zaidi ya wananchi 4,000 wameunganishwa hususani katika maeneo ambayo ni pembezoni mwa mji. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge Dodoma ni kipaumbele na tutaendelea kufanya kazi hiyo kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:- Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) unaendelea kote nchini. Katika Jimbo la Ulyankulu bado umeme haujafika katika maeneo mengi:- (a) Je, ni lini sasa umeme utasambazwa katika Kata za Uyowa, Silambo, Igombe Mkulu, Seleli, Nhwande na Kanoge? (b) Hivi karibuni Wilaya ya Kaliua imesajili Shule za Sekondari tano (5) na Vituo vya Afya pamoja na Sekondari ya Mkondo; je, ni lini sasa umeme utafikishwa katika taasisi hizo?

Supplementary Question 3

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda nami nimuulize Naibu Waziri swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kata zaidi ya sita pale Jimboni kwangu Tarime Vijijini ambapo nguzo zimesimamishwa huu ni mwezi wa nne lakini bado hakuna nyaya wala activity yoyote inayoendelea. Sasa sijui ni nini kinachoendelea na napenda awaambie wananchi ni lini sasa nyaya zitapitishwa pale ili waanze kupata umeme wa REA?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Heche, Mjumbe wetu wa Kamati ya Nishati na Madini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameulizia kuhusu kata sita kwenye jimbo lake ambapo amesema nguzo zimesimama lakini hakuna kinachoendelea. Nimwombe tu Mheshimiwa Heche baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu tukutane ili niweze kufuatilia kwa karibu kwa nini mkandarasi DERM ambaye anaendelea na kazi katika Mkoa wa Mara hafanyi vizuri kwa sababu tunaamini mkandarasi yule ni miongoni mwa wakandarasi sita wanaofanya vizuri. Kwa hiyo, tukutane ili nijue kwa nini katika maeneo hayo bado nyaya hazijasambazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe hofu tu wakazi wa Mkoa wa Mara na nchi nzima, miradi hii tunatarajia mpaka Desemba kazi ya ujenzi wa miundombinu iwe imekamilika, ibaki kazi ya uunganishaji wa wateja ambapo kwa mujibu wa mkataba Mradi wa REA Awamu ya Tatu utakamilika Juni, 2020. Kwa hiyo, niendelee kuwatoa hofu lakini kweli kuna umuhimu wa kuongeza kasi zaidi, tutalifuatilia kwa pamoja ili kujua ni nini kimekwamisha kazi hiyo. Pia napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi karibuni baada ya Bunge hili nina ziara ya Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Nuru Awadh Bafadhili

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:- Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) unaendelea kote nchini. Katika Jimbo la Ulyankulu bado umeme haujafika katika maeneo mengi:- (a) Je, ni lini sasa umeme utasambazwa katika Kata za Uyowa, Silambo, Igombe Mkulu, Seleli, Nhwande na Kanoge? (b) Hivi karibuni Wilaya ya Kaliua imesajili Shule za Sekondari tano (5) na Vituo vya Afya pamoja na Sekondari ya Mkondo; je, ni lini sasa umeme utafikishwa katika taasisi hizo?

Supplementary Question 4

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika eneo la Ilazo, Extension C katika Jiji hili la Dodoma, wananchi wanajenga nyumba zao kwa bidii sana lakini tatizo linakuja kwenye umeme. Wananchi wamefika TANESCO wameambiwa nguzo hakuna na anayetaka nguzo kuanzia nguzo mbili ni Sh.600,000 na kuanzia nguzo tatu na kuendelea inakuwa ni Sh.2,000,000. Hili suala linakuwaje kwa sababu kazi ya Serikali ni kusambaza miundombinu kama walivyofanya Idara ya Maji wamepeleka maji, barabara zimechongwa lakini hili la umeme linakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kujibu swali la nyongeza la mama yangu, Mheshimiwa Nuru. Ameulizia suala la maeneo ya Ilazo hususani swali lake limelenga kwamba wananchi wanakwenda TANESCO wanaambiwa walipie gharama ya nguzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili ni zuri, nataka pia nirejee maelekezo na maagizo ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani kwamba nguzo zote ni bure na kwa nini tumetoa agizo hilo? Gharama ya kupeleka umeme ina vitu vingi; kuna masuala ya transfoma, waya na kadhalika, lakini imekuwa tu ni mazoea kwa Shirika letu la TANESCO kutanguliza kipaumbele cha nguzo wakati ni sehemu tu ya gharama ya kuwaunganishia umeme Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niendelee kusisitiza agizo la Waziri wa Nishati lipo palepale, wananchi waendelee kuhudumiwa kwa TANESCO yenyewe kujiandaa na mpango wa manunuzi wa nguzo kwa sababu zile nguzo zinakuwa mali ya TANESCO. Kwa hiyo, nataka nilichukue suala hili la kulisimamia baada ya kutoka hapa. Kweli nimepokea salamu nyingi sana za wananchi kuhusu kuendelea kwa lugha ya Mameneja kusema nguzo hakuna, kuwachaji wananchi gharama za nguzo na kuwarudisha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tuendelee kusisitiza, tumesema Meneja ambaye hayupo tayari kupanga mipango ya kuwaunganishia wananchi kwa kutumia ubunifu wake kwa gharama za nguzo za Serikali, Meneja huyo atupishe ili tuwape Mameneja wengine mamlaka ili waendelee kuwaunganishia umeme wananchi. Kwa sababu yapo maeneo wanaweza kuunganisha kama kuna maeneo wanaona wanashindwa kutekeleza agizo hili la Serikali yetu ambayo imeamua kuwapunguzia gharama wananchi atupishe tu ili wengine waendelee kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kusisitiza hili agizo lipo na yeyote anayeona hawezi basi atupishe ili tumteue mtu mwingine aweze kupanga mipango ya kuwaunganisha wananchi umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.