Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Felister Aloyce Bura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:- Kutokana na Serikali kuhamia Dodoma, mahitaji ya maji safi na salama yamekuwa makubwa na kwa sasa mgao wa maji kwa wakazi wa Dodoma umeshaanza:- Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuhakikisha wakazi wa Dodoma wanapata maji safi na salama?

Supplementary Question 1

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na shughuli nyingi za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wawekezaji wengi wameamua kuja Dodoma na Serikali yenyewe inakuja Dodoma na vyuo vikuu vingi vinajengwa Dodoma, hasa maeneo ya Nala; na kwa kuwa, maeneo ya pembezoni kama vile Bahi, Wilaya ya Chamwino na maeneo mengine yanahitaji maji kwa ajili ya wawekezaji, je, Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba, hao wawekezaji na wananchi wanaozunguka maeneo hayo hawakosi maji kwa ajili ya matumizi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa, maji ya Ziwa Victoria yameshaletwa mpaka Nzega na kuna taarifa hayo maji yanakuja mpaka Igunga. Je, Serikali haioni kwamba, suluhu ya kudumu kwa ajili ya mahitaji ya Dodoma ni kuleta maji ya Ziwa Victoria ambayo yatasaidia pia Mkoa wa Singida na Dodoma? (Makofi)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze mama yangu Mheshimiwa Felister Bura amekuwa mpiganaji mkubwa sana, hususan kwa changamoto ya maji katika Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, kikubwa ambacho nataka niwahakikishie wakazi wa Dodoma kupitia uongozi mahiri wa kiongozi wetu wa Wizara ya Maji, Profesa Makame Mbarawa, tumekwishaliona hilo. Moja kuwaagiza DUWASA katika kuhakikisha kwenye makusanyo yao ya ndani asilimia 30 wahakikishe wanachimba visima virefu maeneo ya pembezoni ili wananchi wa Dodoma waweze kupata huduma ya maji.

Pili, mpaka sasa tumekwishalipa fidia katika Bwawa la Farkwa kwa wananchi wale ili tuweze kujenga Bwawa la Farkwa. Katika kuhakikisha tunaondoa kabisa tatizo la maji katika Mkoa huu wa Dodoma tumeshaanza kuanzisha timu ya kufanya study ya namna gani ya kuanzisha standard gauge kubwa katika miradi yetu ya maji. Moja ni katika kuhakikisha tunaandaa standard gauge ya kuyatoa maji Ziwa Victoria hadi kuyaleta hapa Dodoma. Subira yavuta heri. Heri itapatikana katika kuhakikisha kwamba, Mradi wa Ziwa Victoria unafikisha maji hapa Dodoma. Ahsante sana.

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTER A. BURA aliuliza:- Kutokana na Serikali kuhamia Dodoma, mahitaji ya maji safi na salama yamekuwa makubwa na kwa sasa mgao wa maji kwa wakazi wa Dodoma umeshaanza:- Je, Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuhakikisha wakazi wa Dodoma wanapata maji safi na salama?

Supplementary Question 2

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Wananchi wa Mji wa Tarime wameendelea kupata adha kubwa ya maji safi na salama na hasa upatikanaji wake. Kupitia Bunge hili nimeshauliza maswali mengi sana na kuchangia na Serikali ikaahidi kwamba, itatoa suluhisho la muda mfupi la kuchimba visima 23 kandokando ya Mji wa Tarime kuweza kuboresha Mradi wa Gamasara na Bwawa la Nyanduruma, lakini zaidi kwenye bajeti iliyopita waliahidi Mradi wa Ziwa Victoria ambao unatokana na mkopo kutoka India kwamba, unaenda kuanza ambao ni suluhisho la muda mrefu.

Sasa napenda kupata majibu kutoka kwa Naibu Waziri, ni lini sasa hii miradi yote inaenda kutengemaa ili wananchi wa Mji wa Tarime waweze kupata maji safi na salama?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, dada yangu Esther Matiko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tulikuwa tuna Mradi pale wa Gamasara ulikuwa ukifanya kazi kwa kusuasua, nilifika na tumechukua hatua kubwa ya kushughulikiana na yule mkandarasi. Wiki hii tunafunga pampu ili kuhakikisha wananchi wale wanapata huduma hii ya maji, lakini tunatambua kabisa Mkoa wa Mara ni maeneo yenye changamoto.

Mheshimiwa Spika, tumepata fedha takribani kwa mikoa 17 mmojawapo ukiwa Mkoa wa Mara na tumekwishatuma fedha zaidi ya Sh.8,345,000,000. Katika jimbo lake mpaka sasa tumekwishatuma pesa zaidi ya Sh.1,345,000,000, hizo fedha ni kwa ajili ya utekelezaji. Kwa hiyo, hizo fedha ziende zikatumike katika kuhakikisha zinachimba visima katika maeneo yenye changamoto ili wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, pia katika kuhakikisha tunatatua kabisa tatizo la maji Rorya pamoja na Tarime ni moja ya maeneo ambayo tumeyaweka katika miji 28 kupitia fedha za India. Tunasubiri kibali kutoka Exim Bank ili tuweze kutangaza tenda kwa ajili ya kuwapata wakandarasi na Mradi ule mkubwa wa kuyatoa maji Ziwa Victoria ili wananchi wa Tarime waweze kupata huduma ya maji. Ahsante sana.