Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Albert Ntabaliba Obama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Primary Question

MHE. ALBERT O. NTABALIBA aliuliza:- Walimu wa hesabu na sayansi ni changamoto kubwa ndani ya Wilaya ya Buhigwe:- (a) Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu katika wilaya hiyo na waliopo sasa ni wangapi? (b) Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa vya maabara katika shule za Buhigwe?

Supplementary Question 1

MHE. ALBERT N. OBAMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nishukuru majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni ukweli kwamba tuna upungufu mkubwa nchi nzima wa Walimu wa sayansi na hesabu na kwenye jibu lake la msingi ameonesha kwamba Buhigwe ina upungufu wa asilimia 46. Sasa na hiki kimekuwa ni kikwazo ambacho kinatufanya kwamba ufaulu wetu uwe mdogo na kule ni pembezoni, kwamba watoto hawawezi kupata namna ya kuweza ku--access namna ya kujisomea kwa kufundishana. Je, ni lini itaweka umuhimu wa kuongeza Walimu wa sayansi katika Wilaya ya Buhigwe?

Mheshimiwa Spika, la pili nipongeze wananchi wa Wilaya ya Buhigwe kwa juhudi na kujitolea kujenga maabara na kujenga madarasa. Je, ni lini Serikali italeta sasa vifaa vya maabara kwa sababu tunaendelea kukamilisha sasa maabara katika shule nyingine, ni lini italeta vifaa hivyo kwa wanafunzi?

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nijibu mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Obama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna upungufu wa Walimu wa masomo ya sayansi na hisabati na kama nilivyoongea kwenye jibu langu la msingi ni kwamba sasa hivi tunafanya mchakato wa kumalizia kuajiri Walimu zaidi ya 4,500 na tumeyaweka mahsusi kabisa kwamba maeneo haya, Wilaya yako ya Kongwa, kule Buhigwe na maeneo mengine, tutazingatia maeneo ambayo yana upungufu mkubwa zaidi.

Tunaomba tupate taarifa kwa sababu kuna mahali unakuta kweli shule nzima haina hata Mwalimu wa hesabu, au baiolojia, kemia au fizikia, tutaweka vipaumbele maeneo hayo ambayo yana changamoto kubwa. Hii ni awamu ya kwanza ya ajira, awamu ya pili ikipatikana pia tutakuwa tunapeleka Walimu kadri uwezo utakavyokuwa unapatikana.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anauliza habari ya kumalizia maboma ya maabara. Nimesema kwenye majibu yangu ya msingi ni kwamba tayari hapa tulipo tunasambaza vifaa, tenda imeshatangazwa, kazi inafanyika. Inawezekana wakati tunaomba taarifa kwenye halmashauri mbalimbali labda watu wetu kule hawakuleta taarifa hiyo. Kwa hiyo Mheshimiwa Obama kama ana wasiwasi kwa hili la kupeleka vifaa vya maabara kwenye eneo lake, basi naomba tuwasiliane ili tuweze kuzingatia maombi yake. Ahsante.