Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Innocent Sebba Bilakwate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyerwa

Primary Question

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:- Baada ya Serikali kukamilisha usanifu wa mradi wa maji wa vijiji 57 kwenye kata 15 Wilayani Kyerwa:- Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwenye Bajeti ya 2019/2020 ili miradi hiyo ianze kutekeleza Ilani ya CCM ya kumtua mama ndoo kichwani?

Supplementary Question 1

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa hatua ambayo imefikia kwenye usanifu, lakini niombe kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa sababu ya hali ngumu kwa wananchi wa Jimbo la Kyerwa hasa hasa kwenye vijiji ambavyo vinaguswa na mradi huu, je, Serikali iko tayari kwenye bajeti ya 2019/2020 kutenga angalau kiasi kidogo ili mradi huu uweze kuanza wakati Serikali inaendelea kutafuta hela kubwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna miradi ambayo iko katika Kata ya Mabira, Lukulaijo na kwenye Kijiji cha Kageni miradi hii imeshaanza lakini wakandarasi wamekuwa wakienda kwa kusuasua kwa sababu bado certificate zao hazijalipwa. Je, Serikali iko tayari kuwalipa wakandarasi hawa ili waweze kukamilisha hii miradi?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Bilakwate, mimi binafsi nilipata nafasi ya kwenda katika jimbo lake, nimeona kazi kubwa anayoifanya katika jimbo lake pamoja na wananchi wake. Sasa nataka nimhakikishie sisi kama Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo kwa wananchi wa Kyerwa kupata maji safi salama na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Spika, tumefanya tathmini ule mradi ni fedha nyingi sana, lakini tunatambua maji ni uhai na hayana mbadala. Sasa nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ukikosa ziwa la mama, la ngombe unanyonya, sisi tupo tayari kufanya njia mbadala katika kuhakikisha wananchi wake wa Kyerwa wanapata maji safi na salama ili waweze kuishi katika eneo lake. Kikubwa na cha msingi kabisa nimwombe kutokana na kuna miradi ambayo inaendelea katika jimbo lake, tukutane baada ya saa saba ili tuangalie ni namna gani tunamsaidia katika kuhakikisha fedha zile tunazilipa wananchi wake waweze kupata maji safi.