Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Primary Question

MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:- Wananchi wa Vijiji vya Hurumbi, Dumi na Chandimo Kata ya Serya, Ausia, Mulua na Guluma (Suruke) pamoja na Hachwi, Kutumo na Chora (Kolo) katika Jimbo la Kondoa Mjini, kijiografia wana changamoto kubwa ya huduma muhimu za afya ambapo wanalazimika kufuata huduma hizo katika zahanati za jirani au hospitali ya mjini:- Je, ni lini Serikali itatupatia Mobile Clinic kutatua changamoto hii?

Supplementary Question 1

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Hapa naweza nikasema ni pale ambapo Golikipa wa Simba anapigiwa shuti la penati na mshambuliaji wa Yanga halafu yeye anaenda kushoto goli linaingia kulia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, majibu yaliyotolewa na Serikali pamoja na shukrani zote, lakini kidogo yamekwenda tofauti na malengo ya swali lenyewe. Huu utaratibu wa Hospitali Tembezi tumekuwa tukiufanya hasa sisi wenyewe Wabunge tukishirikiana na Ofisi ya Mkoa. Tumefanya mara kadhaa, kama mara tatu na tunatarajia tena mwezi wa Septemba, 2018 tutapata nyingine kutoka Marekani.
Mheshimiwa Spika, nilichokuwa nikitarajia hapa ni ubunifu huu tulioanza nao kutokana na uchache wa huduma za kibingwa lakini pia na huduma nyingine za afya, kwenye ngazi ya Halmashauri na kwenye ngazi ya Wilaya tuupeleke kwenye vijiji, ndiyo maana niliainisha vijiji vingi ambavyo tunavizungumzia hapa.
Mheshimiwa Spika, kwa kawaida tumekuwa tunachukua gari la chanjo na mengineyo ya miradi kufikisha huduma za kliniki za watoto, chanjo, huduma za akinamama wale, lakini sasa zinafanyika nje kwenye uwazi, jambo ambalo halina staha sana, ndiyo maana tukawa tunahitaji Kliniki Tembezi. Huu ni ubunifu tuliofanya kwenye ngazi ya Wilaya, sasa tuufanye kwenye ngazi ya Vijiji. Je Serikali haioni umuhimu wa kuenzi na kuiga ubunifu huu kwenye ngazi ya vijiji? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuweza kujenga Zahanati kwenye kila Kijiji kama ilivyo sera yetu, gharama yake ni kubwa sana na haya maeneo yote niliyoainishwa unaweza ukazungumzia maeneo matano mpaka sita ambapo ukipata gari moja la namna hiyo la Kliniki Tembezi, linaweza likakusaidia kuweza kumaliza huduma ya kujenga Zahanati nne. Je, ni lini basi, na kwa kuwa tunafahamu uwezo wetu ni mdogo bora tufanye...
Eeh! Mheshimiwa Spika, ni lini basi, Serikali itaiga ubunifu huu na kutuletea Mobile Clinic Van kwa ajili ya maeneo yetu ya Kondoa? (Makofi

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu kwanza nimpongeze Mheshimiwa Sannda kwa jinsi ambavyo amekuwa akipigania wananchi wake kuhusiana na suala zima la afya. Wiki iliyopita alikuwa anaongelea juu ya suala la gari la wagonjwa, lakini leo anaongelea juu ya Mobile Clinic.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake alilenga gari linalotembea kwa ajili ya kutoa huduma. Sasa kwa namna ambavyo swali limekuja ndiyo maana anasema ni kama tumehamisha goli, lakini siyo nia ya Serikali kuhamisha magoli kwa sababu majibu yote tunayo.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza anauliza uwezekano wa kuiga hili jambo zuri ili kuvipunguzia vijiji vingi badala ya kufuata huduma maeneo ya mbali. Naomba tukubalianae na Mheshimiwa Sannda kwamba ni nia ya Serikali, pale ambapo uwezo unakuwa umeruhusu hatuna sababu ya kutowapelekea wananchi huduma jirani yao.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anaomba tuige utaratibu mzuri ili kuwa na Mobile Clinic Van. Utakubaliana nasi kwamba wananchi wengi wamejitokeza, wametoa nguvu zao katika ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya. Pamoja na wazo jema hili, lakini itakuwa siyo busara nguvu ile ambayo imetumiwa na wananchi tukai-dump halafu tukaanzisha jambo lingine. Kwa kadri nafasi itakaporuhusu na nguvu ya kibajeti ikiruhusu, wazo hili ni jema, naomba tulichukue kama Serikali kulifanyia kazi kwa siku za usoni. (Makofi)

Name

Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:- Wananchi wa Vijiji vya Hurumbi, Dumi na Chandimo Kata ya Serya, Ausia, Mulua na Guluma (Suruke) pamoja na Hachwi, Kutumo na Chora (Kolo) katika Jimbo la Kondoa Mjini, kijiografia wana changamoto kubwa ya huduma muhimu za afya ambapo wanalazimika kufuata huduma hizo katika zahanati za jirani au hospitali ya mjini:- Je, ni lini Serikali itatupatia Mobile Clinic kutatua changamoto hii?

Supplementary Question 2

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mazingira yaliyopo Kondoa yanafanana na mazingira yaliyopo Babati Vijijni. Zahanati ya Galapo ni Zahanati ya muda mrefu, imepandishwa kuwa Kituo cha Afya, lakini mpaka sasa hatuna jengo la upasuaji. Kwa nguvu za wananchi tumejitahidi mpaka tumepaua hilo jengo. Mpaka sasa tuna vifaa vya hicho chumba cha upasuaji lakini tuna changamoto ya kumalizia hilo jengo ili litumike. Ni lini sasa Serikali itapeleka pesa za kumalizia hilo jengo? (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeze dada yangu Mheshimiwa Anna kwa swali zuri, lakini nawapongeza Wabunge wa Babati na kaka yao Mheshimiwa Jitu Soni kwa pamoja. Nafahamu Babati Vijijini ina changamoto kubwa ya afya na ndiyo maana kwa Zahanati ya Galapo ambayo imepandishwa lakini kwa sasa kipaumbele chetu kwamba tumeanza na vituo viwili vya afya, kile ni cha kwanza na sasa hivi tunaenda katika Kituo cha Magugu, kwa sababu tunajua pale Magugu ni center kubwa sana gari nyingi zinapita.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo tumeweka kipaumbele na hata hivyo ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Kituo cha Afya cha Galapo tutafanya kila liwezekanalo kwa mipango ya Serikali tuweze kukiimarisha kwa ajili ya wananchi wa Babati Vijijini waweze kupata huduma vizuri. (Makofi)

Name

Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Primary Question

MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:- Wananchi wa Vijiji vya Hurumbi, Dumi na Chandimo Kata ya Serya, Ausia, Mulua na Guluma (Suruke) pamoja na Hachwi, Kutumo na Chora (Kolo) katika Jimbo la Kondoa Mjini, kijiografia wana changamoto kubwa ya huduma muhimu za afya ambapo wanalazimika kufuata huduma hizo katika zahanati za jirani au hospitali ya mjini:- Je, ni lini Serikali itatupatia Mobile Clinic kutatua changamoto hii?

Supplementary Question 3

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa matatizo yaliyoelezwa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu ni sawa kabisa na matatizo yaliyoko Jimboni kwangu. Jimbo la Geita Vijijini lenye population ya watu kama 1,000,000 halina kabisa Kituo cha Afya hata kimoja, baada ya Kituo cha Afya Nzela kupanda hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya. Je, Wizara haioni umuhimu wa kutusaidia pesa ili tuweze kujenga kituo kwa wananchi walioko Ibisabageni na Rubanga kuliko na umbali wa kilometa 80 mpaka kukipata Kituo cha Afya kilichopandishwa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya? (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kweli tunafahamu changamoto kubwa ya afya kule Geita Vijijini na hata hivyo namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kwa pamoja tumeshirikiana kuhakikisha Kituo cha Afya cha Nzela kile cha kwanza kimekuwa ni cha kisasa zaidi. Hata hivyo, kwa vile tunajua changamoto ni kubwa, ndiyo maana Geita DC sasa hivi tunaenda kuipa Hospitali ya Wilaya rasmi sasa katika bajeti yetu ya mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika Mpango wa Serikali wa sasa, nia yetu ni kwamba kabla ya mwezi wa Tisa mwishoni kuelekea mwezi wa Kumi tutakuwa tumeweka miundombinu ya kisasa katika Kituo cha Afya cha Nyarugusu, nadhani ni Zahanati lakini tutai-upgrade. Lengo kubwa ni kwamba wachimbaji ambao ni population kubwa ya eneo lile waweze kupata huduma nzuri sana ya afya na kuwahudumia wananchi wa Geita kwa ujumla wake. (Makofi) Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Name

Dr. Mary Michael Nagu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Primary Question

MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:- Wananchi wa Vijiji vya Hurumbi, Dumi na Chandimo Kata ya Serya, Ausia, Mulua na Guluma (Suruke) pamoja na Hachwi, Kutumo na Chora (Kolo) katika Jimbo la Kondoa Mjini, kijiografia wana changamoto kubwa ya huduma muhimu za afya ambapo wanalazimika kufuata huduma hizo katika zahanati za jirani au hospitali ya mjini:- Je, ni lini Serikali itatupatia Mobile Clinic kutatua changamoto hii?

Supplementary Question 4

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii adimu. Wilaya ya Hanang’ ina Kituo cha Afya kimoja ambacho ndicho kinakarabatiwa sasa lakini kuna Wilaya kubwa haina Kituo cha Afya kingine. Nilimwomba Mheshimiwa Waziri Kituo cha Afya cha Basotu na Kituo cha Afya cha Endasak ambako kuna watu wengi ambao wanategemea huduma hiyo, atusaidie. Je, anaweza kutuambia ni lini ukarabati huo utaanza ili watu wa Endasak na Basotu waweze kunufaika na huduma ya afya? Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba nikiri kwamba Mheshimiwa Mary Nagu, tena alikuja na wananchi wake tukiwa getini alileta hiyo hoja. Nakiri wazi pia kwamba Endasak na Basotu ni changamoto kubwa na ina population kubwa. Nia na mpango wa Serikali ni kwamba Mungu akijaalia kabla ya mwezi wa Tisa tutakuwa tumeshaanza ujenzi pale Basotu kwa kadri kama tulivyokubaliana siku ile. (Makofi) Mheshimiwa Spika, nashukuru.