Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ester Michael Mmasi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER M. MMASI (K.n.y. MHE. ESTER A. MAHAWE) aliuliza:- Gharama za kupanda Mlima Kilimanjaro ni mara mbili ya gharama za kupanda Mlima Kenya; hali hii imesababisha kushuka kwa idadi ya watalii na kuinyima Serikali mapato. Je, ni lini Serikali itafanya marekebisho ya bei hizo?

Supplementary Question 1

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa background information nzuri sana. Kimsingi nioneshe tu masikitiko yangu kwamba ukiangalia muktadha wa swali hili, itoshe tu kusema kwamba bado Mheshimiwa Waziri hakuweza kulitendea haki swali hili.
Mheshimiwa Spika, swali liliuliza; je, ni lini Serikali itafanya marekesho ya bei hizi katika kuimarisha uchumi wa Taifa hili na hususan wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro? Ingekuwa swali linauliza je, Serikali ina mkakati gani? Ndipo jibu lilipaswa kuwa hili. Kwa sababu jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri linasema Serikali imejinga kukutana na wadau. Ni kweli, lakini swali lililenga kujua ni lini hasa?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni kweli kwamba moja ya kuinua mapato ya Serikali kupitia kivutio hiki cha Mlima wa Kilimanjaro ni pamoja na kuboresha mpango mkakati wa soko la utalii duniani. Nilipenda Mheshimiwa Naibu Waziri atuambie, je, kupitia uwekezaji wa Shirika la Ndege la Tanzania ni kwa nini Serikali haikuona umuhimu wa kurudisha nembo ya Mlima wa Kilimanjaro katika ndege hizi za Shirika la Ndege ili basi kwa muktadha huo tuweze kuinua soko la utalii kwa nchi ya Tanzania? Ahsante. (Makofi)

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza. Najua yeye ni mdau mkubwa sana katika huu mlima na amekuwa akitushauri sana katika masuala mengi. Kuhusu maswali yake yote mawili ambayo ameuliza, suala la kuuliza ni lini? Labda nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge tumeshakutana na wadau mbalimbali katika kuzungumza masuala mbalimbali zikiwemo changamoto pamoja na gharama kubwa ambazo wanatozwa watu mbalimbali wanaopanda Mlima Kilimanjaro. Tumeshakaa tumezungumza, lakini kama Serikali tunataka kujiridhisha. Tunataka tukutane na wadau wengi zaidi kuliko wale wa vyama vyao ili tuone kama kuna haja ya kupunguza au hakuna haja ya kupunguza.
Mheshimiwa Spika, suala la kwamba ni lini? Basi niseme tu kwamba kati ya kipindi cha sasa mpaka mwezi Desemba, hili suala tutakuwa tumeshafikia muafaka kama tupunguze au tuongeze. Kwa hiyo, siyo suala la kupunguza tu.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba kulikuwa na nembo kwenye Shirika la Ndege zetu la Kilimanjaro, nadhani tulikuwa na alama kwa ajili kutangaza Mlima wetu Kilimanjaro. Ilikuwemo kwenye nembo hiyo na bado itaendelea kuwemo. Mpaka sasa hivi tumeweka zaidi, lakini siyo tu kutangaza Mlima Kilimanjaro, bali tunaangalia na vivutio vingine vingi ambavo vipo, ndiyo maana ndege zetu sasa hivi tunaweka vitu vingi na alama nyingi zaidi ambazo zinaendelea kulitambulisha Taifa letu. Bado tutakaa na wadau mbalimbali kuona kama kuna haja ya kurudisha ile alama iwepo pale kama alama ya utambulisho. (Makofi)

Name

Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Primary Question

MHE. ESTER M. MMASI (K.n.y. MHE. ESTER A. MAHAWE) aliuliza:- Gharama za kupanda Mlima Kilimanjaro ni mara mbili ya gharama za kupanda Mlima Kenya; hali hii imesababisha kushuka kwa idadi ya watalii na kuinyima Serikali mapato. Je, ni lini Serikali itafanya marekebisho ya bei hizo?

Supplementary Question 2

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Aaah, ni mimi bwana.
Nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nakubaliana na Mheshimiwa Waziri kwamba gharama za kupanda Mlima Kenya haziwezi kulingana na Mlima Kilimanjaro kwa sababu ya unique tuliyonayo katika mlima wetu. Tumezungumza na tour guides ambao wanafanya hiyo kazi, wanasema hiyo siyo sababu; sababu ni kuongezeka kwa 18 percent ya VAT katika gharama ambayo inamgusa moja kwa moja mtalii.
Je, Serikali lini sasa itakaa kuona kwamba hili ni tatizo na kuonda 18 percent kwa wageni wanaokuja ili waje kwa wingi na tukusanye kwa wingi? (Makofi)

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ni kweli kabisa kwamba Serikali ilianzisha VAT katika huduma mbalimbali za kitalii ambazo zinatolewa, ni karibu takribani miaka miwili sasa imepita toka kuanzishwa kwa VAT.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuliagizwa tufanye utafiti mpana zaidi tuone kama kweli hii VAT imeleta athari. Sasa katika kipindi kifupi ni vigumu sana kuweza kujua kama VAT imeleta athari au haijaleta athari. Kwa hiyo, sasa hivi ambacho tunakifanya, tunataka tufanye study kubwa, lakini pia tuone ni maeneo gani ambayo tunaweza kuyatumia ambayo tunaweza kupanua wigo wa kupata mapato mengi zaidi badala ya kutegemea tu suala la VAT.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili tutalifanyia kazi na tunaomba tuendelee kupata maoni zaidi na mawazo namna ya kuboresha huduma zetu hizi za utalii.