Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Primary Question

MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:- Wananchi wa Kata ya Nkandasi wamejitahidi kujenga Shule ya Sekondari ya Kata ya Milundikwa hadi kufikia Kidato cha Sita, lakini Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeamua shule hiyo kuhamishwa mara moja kuanzia tarehe 1 Januari, 2017 ili kuliachia Jeshi:- (a) Je, Serikali inatoa mchango gani katika uhamishaji na ujenzi mpya wa shule hiyo? (b) Je, Serikali iko tayari kufanya tathmini ya miundombinu yote ya shule na majengo yaliyojengwa na wananchi na thamani hiyo kuitoa katika fedha taslimu kwa ujenzi mpya wa shule?

Supplementary Question 1

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nakiri kwamba ni kweli Jeshi la Kujenta Taifa wametusaidia na wanaendelea kutusaidia hata katika kazi nyingine, lakini wakati shule hii inatwaaliwa ilikuwa na miundombinu mingi sana na sasa miundombinu bado haijarejeshwa yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shule hii sasa haina nyumba hata moja ya Mwalimu na ukizingatia kwamba ina Kidato cha Tano na Sita ambayo ni boarding ni wasichana wanakaa peke yako. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuendelea kutupatia pesa zaidi na hasa pesa za kujenga nyumba za Walimu ambapo sasa hivi hakuna hata nyumba moja?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili wakati Serikali inatwaa eneo hili na kuipatia Jeshi limezuka suala lingine ambalo ni gumu zaidi. Wanajeshi walipokuja pale wamechukua eneo sasa la mashamba wanayolima wananchi na kufanya wananchi zaidi ya elfu tano wa Vijiji vya Kasu, Milundikwa, Kisula na Malongwe zaidi ya elfu nne kukosa mahali kabisa pa kulima. Naiomba Serikali je, iko tayari kufikiria upya na wakati mwingine ione uwezekano wa kuwagawia wananchi sehemu ya eneo ili waendelee kuendeleza maisha yao? (Makofi)

Name

Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Wizara yangu iko tayari kuendelea kusaidiana, kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya katika kutoa vifaa vya ujenzi ili waweze kukidhi mahitaji yao ya kuifanya shule hii ipate miundombinu inayotakiwa. Bila shaka kutakuwa kuna bajeti za kawaida za kupitia Halmashauri nazo hizo wakizielekeza huko na sisi tutakuwa tayari kutoa mchango wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Serikali kutwaa eneo hili na kufanya watu wengi karibu elfu nne kukosa sehemu ya kulima nataka nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali haijalitwaa eneo hili bali eneo hili lilikuwa ni mali ya Serikali mali ya JKT toka mwanzoni. Kama wakati wa JKT kurudi pale imetokea kwamba eneo lililochukuliwa ni zaidi ya lile la awali hilo naweza nikalingalia, lakini ukweli ni kwamba taarifa tulizokuwa nazo ni kwamba JKT wamekwenda kuchukua eneo lao la awali walilokuwa nalo kabla ya mwaka 1994 kusitisha shughuli za JKT.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge tukae ili tulijadili suala hili na ikiwezekana tufanye ziara pale tuone tunaweza kusaidia vipi. (Makofi)