Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Primary Question

MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:- Kata ya Sigino na Vijiji vyake vyote katika Jimbo la Babati Mjini haina kabisa maji safi na salama:- Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuipatia maji safi na salama Kata hiyo pamoja na Vijiji vyake?

Supplementary Question 1

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ni kweli majibu hayo aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri ni ya kweli kabisa kwa hatua ambazo zinaendelea katika Halmashauri, lakini huyu Mkandarasi Maswi kimsingi amekuwa akitusumbua sasa muda mrefu kweli amekuwa akitoa sababu mbalimbali kwamba sijui ni masika hawezi kutafuta haya maji. Sasa naomba kwa sababu ilikuwa ni commitment ya Waziri wa Maji alifika katika Kata hii na katika kijiji hiki, je, Wizara hii pamoja na Wizara ya Maji wanaweza wakatupa ushirikiano DDCA wakatusaidia, kwa sababu wao wanafahamu ni wapi maji yanapatikana badala ya huyu Maswi akaendelea kutusumbua na wananchi wale wakapata maji?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nakubaliana na Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba huyu Mkandarasi wa awali anayechimba maji katika Kijiji cha Imbilili kwa kweli amekuwa akitusumbua sana, lakini hayo tutayafanyia kazi kwenye Baraza letu kama alivyoshauri. Naomba nifahamu Wizara iko tayari sasa kuangalia bili tunazolipa za maji katika Mji wetu wa Babati kwa sababu wananchi wetu wakilalamika sana, pamoja na upungufu wa maji lakini wanatozwa bili kubwa sana za maji. Je, Wizara hii na Wizara ya Maji mko tayari ku-review bili ambazo wananchi wa Babati wanalipa?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kitaalam ni kweli kwamba huwezi kufanya utafiti mpya wa maji chini ya ardhi hasa kama unataka kuchimba visima wakati huu wa masika. Kwa hiyo, kama Mkandarasi ameomba muda kidogo apewe ambapo yupo asilimia 25 kwa sasa hivi, kama anapewa muda wa mwezi wa Tano anaweza akachukua muda wa mwezi mmoja kumalizia visima vile ambavyo alikuwa anachimba kwenye vile vijiji na ikiwezekana mwezi wa Sita au mwezi wa Saba akamaliza kazi ya kuchimba visima. Nashauri kitaalam apewe muda wa mwezi wa Tano na Sita ili kusudi aweze kukamilisha kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Spika, kama Mkandarasi huyu Maswi ataondolewa sasa hivi halafu wakaanza mchakato mpya wa kumpata kazi mtu mwingine wanaweza wakachukua miezi sita kukamilisha kumpata Mkandarasi ambayo itakuwa ni siyo faida sana kwa wananchi. Kwa hiyo, nashauri avumiliwe kidogo kwa kipindi hiki cha miezi miwili ama mitatu ili aweze kukamilisha kazi yake. Wizarani tutasukuma ili kusudi aweze kufanya kazi yake kitaalam zaidi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ningependa kuisifu sana Mamlaka ya Maji Mjini Babati, kama ambavyo imesifiwa pale ambapo Waziri Mkuu alienda mwaka juzi waliisifu wao wenyewe BUWASA kwamba inafanya kazi nzuri na hata Mheshimiwa Diwani Sumaye ambaye anatoka kwenye Kata ile ya Sigino ambako hakuna maji kabisa, mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kwamba bwana kwa kweli tunashukuru wenzetu wa Mjini Babati wanapata maji vizuri, tatizo hapo ni bili.
Mheshimiwa Spika, ili kusudi ianzishwe bili, EWURA kabla hawajaidhinisha huwa wanafanya kitu kinaitwa mkutano wa wadau, wanajadili, wakishakubaliana wadau ndiyo bili ile inaidhinishwa. Kwa hiyo, nashauri Halmashauri kama inaona kwamba bili ni kubwa basi wawasiliane na EWURA kwa barua rasmi ili kusudi suala hilo liweze kutatuliwa. Mheshimiwa Spika, ahsante.