Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Leonard Haule

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mikumi

Primary Question

MHE. JOSEPH L. HAULE (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:- Je, Serikali ina mikakati gani ya muda mrefu katika kuimarisha ushiriki wenye tija kwa Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote naomba nitoe pole sana kwa familia za wasanii wenzangu, Jebby Mubarak na Agnes Gerald Masogange ambao wametangulia mbele za haki. Mungu awalaze mahali pema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba moja, pamoja na jitihada hizo tunazoziona za watu mmoja mmoja, wanariadha kuweza kufanya vizuri katika michezo mbalimbali, lakini imekuwa tabia ya Watanzania kupeleka timu mbaimbali kwenye mashindano mengine bila kuwaandaa.
Je, kwa nini sasa Serikali isiache kuwapeleka kwanza wanamichezo hao huko nje mpaka ihakikishe imewaandaa na kuweza kufanikiwa kuleta medali na kuitangaza vizuri Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba mbili, changamoto kubwa ya wanamichezo wa Tanzania ni viwanja kukosa ubora na nadhani ile shilingi trilioni 1.5 ingeweza kupunguza kwa kiasi kikubwa sana changamoto hiyo. Mara baada ya mfumo wa chama kimoja kusitishwa mwaka 1992 Chama cha Mapinduzi kimeonekana kuhodhi viwanja vikubwa karibu vyote vikubwa hapa nchini na kushindwa kuviendeleza…

MHE. JOSEPH L. HAULE: Je, hamuoni kwamba huu ni wakati muafaka sasa wa Chama cha Mapinduzi kurudisha viwanja vya michezo hivyo Serikalini ili viweze kutumika na Watanzania wote kwa ujumla? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa maswali mazuri ambayo yameulizwa na kaka yangu Profesa Jay. Nikianza na swali lake la kwanza ambapo ametoa ushauri kwamba kwa nini Serikali haipeleki wanamichezo nje kwa ajili ya kwenda kufanya maandalizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba ushauri ambao ameutoa ni mzuri lakini nachukua pia nafasi hii kuweza kumtoa hofu kwamba katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 kwa sababu sisi kama nchi tunajua kabisa vijana wetu wa Serengeti Boys wanakabiliwa na mashindano makubwa na AFCON ambayo Tanzania itakuwa ni mwenyeji mwaka 2019. Kwa hiyo sisi kama Serikali kwa kushirikiana na TFF tuko kwenye mpango wa kuwachukua vijana wetu kuwapeleka Sweden kwa ajili ya kwenda kupata hayo mazoezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili ambapo amedai kwamba viwanja vingi vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi, niseme kwamba imekuwa ni Sera ya Michezo ya mwaka 1995 kuhamasisha wadau wote kuwa vyama vyote na taasisi zote vina hali ya kuweza kumiliki viwanja vya michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, viwanja vyote ambavyo vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi vinamilikiwa kwa halali na ni haki yao na hakuna hata kiwanja kimoja ambacho kimeporwa na Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nachukua nafasi hii kuweza kuhamasisha Wabunge wote ambao mpo ndani ya Bunge hili, Halmashauri zote, wadau na taasisi zote kuhakikisha kwamba vinatenga maeneo kwa ajili ya michezo kwa sababu ni sera yetu ya mwaka 1995. Ahsante. (Makofi)