Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MEH. RISALA S. KABONGO aliuliza:- Utekelezaji wa Tangazo rasmi la Serikali la Mwaka 2008 juu ya mpaka mpya wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika Bonde la Usangu umeshindikana, hivyo kufanya upanuzi holela wa maeneo ya kilimo, uvamizi wa mifugo mingi na matumizi holela ya maji katika kilimo, jambo ambalo limesababisha uharibifu wa mazingira, Mto Ruaha Mkuu kuendelea kukauka kila mwaka na kuathiri uzalishaji umeme katika Bwawa la Mtera na Kidatu na shughuli zingine na matumizi ya maji ya Mto Ruaha Mkuu:- (a) Sababu zipi za msingi zilizosababisha utekelezaji wa Tangazo hilo kushindwa kwa takribani miaka nane sasa? (b) Je, Serikali inachukua hatua gani za haraka ili kunusuru na kusitisha uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea katika Bonde la Usangu?

Supplementary Question 1

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza, naitwa Risala Said Kabongo siyo Kabogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu mwaka hadi mwaka kunasababisha athari za kimazingira na athari za kukua kwa utalii katika hifadhi hiyo, pamoja na athari kwa wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi hiyo.
Swali la kwanza, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Mto Ruaha Mkuu ambao ndiyo kiini cha hifadhi ya Ruaha unatiririsha maji yake mwaka mzima?
Swali langu la pili, je, Serikali itawasaidiaje wananchi wanaoishi kandokando ya bwawa la Mtera ambao uchumi wao unategemea uvuvi na kilimo kupitia mto huu wa Ruaha. Ahsante.

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimwombe radhi kwa kutamka jina lake ndivyo sivyo, nimepokea masahihisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mkakati, Serikali inao mkakati siyo kuhusu tu eneo la Bonde la Usangu na Mto Ruaha Mkuu, Serikali inao mradi mkubwa kabisa ambao unakusudia kuboresha shughuli za utalii kwenye eneo la Kusini, mradi ambao unatamkwa kwa kifupi re-grow yaani the Resilient Natural Resources Management for Growth.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huo eneo la Bonde la Usangu ambalo linajumuisha Mto wa Ruaha ni sehemu ya mradi huu. Tunakwenda kuboresha mambo yote yanayohusiana na uhifadhi katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba eneo hilo lote sasa linakuwa na sifa endelevu ya kuwa na kila kitu kilichomo ndani yake katika hali ya uhifadhi unaotambulika Kimataifa na unaokubalika katika kuwezesha shughuli za utalii ziendelee kubaki kuwa bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, mradi huu ambao unatekelezwa chini ya Benki ya Dunia sasa hivi upo katika hatua za awali katika siku zijazo za usoni tutautolewa taarifa kuhusiana na jinsi ambavyo tutakuwa tunaendelea kuboresha eneo ambalo nimelitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wananchi wa Mtera inafanana na jibu nililojibu kwa ujumla kwamba mradi huo ninaoutaja ambao upo chini ya Benki ya Dunia unajumuisha mambo yote, yakiwemo kuhifadhi mito iliyomo ndani yake, kuhifadhi misitu iliyopo ndani yake, pia kuangalia maisha ya binadamu na shughuli zao katika eneo linalohusika kama wafugaji, wakulima na wengine wanaofanya shughuli nyingine zote watajumuishwa katika malengo makuu ya mradi huu na kwa hiyo maslahi yao yatazingatiwa Kitaifa katika mradi huo.