Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Primary Question

MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:- Kijiji cha Nyakanazi, Wilaya ya Biharamulo kiko kwenye njia panda kwenda Kigoma, Kahama, Ngara na kina wakazi wapatao 15,000. Kulingana na hali hiyo, kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinaibuka na idadi ya watu inaongezeka kwa kasi; aidha, kijiji hicho pia kimebanwa na hifadhi inayopakana nacho. Je, Serikali ipo tayari kujadiliana na Halmashauri ya Wilaya na wakazi wa Nyakanazi ili kuona uwezekano wa upanuzi wa eneo la kijiji kwa upande wa hifadhi inayopakana na kituo cha polisi kwa nia ya kufungua fursa za kiuchumi?

Supplementary Question 1

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Kwa kuwa Nyakanazi ni eneo lililokaa kimkakati kwa maana ni njia panda ya kuelekea Kigoma, Kahama na nchi za jirani za Rwanda na Burundi na kwa kuwa hivi karibuni kulingana na mipango ya Serikali iliyopo, kutakuwa na reli inatoka Isaka kwenda Rwanda.
Je, Naibu Waziri haoni kwamba sambamba na mchakato unaopaswa kufanywa na kijiji kupitia Halmashauri na Mkoa, Serikali Kuu nayo ina wajibu wa kuingia kwenye mchakato huo ili nguvu hizo zikutane kupaboresha zaidi kwa sababu panaendelea kuwa sehemu ya mkakati ikiwekwa reli?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuambatana nami atakapopata fursa ili twende kuona kwa pamoja na kufanya maandalizi ya kifikra kabla hata mchakato wa vikao haujaanza? Nakushukuru sana.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niungane na Mheshimiwa Mbunge kwamba pale Nyakanazi ukiangalia kijiografia, ndiyo unapata njia ya kwenda Kakonko kule, lakini inaondoka Rwanda na huku tena inaenda Bukoba yaani ni junction pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale kweli ukuaji wake ni mkubwa sana, ndiyo maana hata mwaka huu katika usajili wa watoto peke yake, inaonekana darasa la kwanza tumesajili zaidi ya wanafunzi 1,000 na kitu katika shule ya Nyakanazi. Kwa hiyo, mahitaji ni makubwa, lakini baada ya kuongea na viongozi pale, kuna mpango mkakati kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge siku nilivyofika pale, ni kwamba wanataka kuifanya kuwa hub fulani ya kibiashara kubwa sana kwa ajili ya kufanya mji ule kuwa chemchem.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la kuungana na wananchi wa pale, kama Serikali Kuu tumesema kwamba kama hilo litafanyika vizuri na Waziri mwenye dhamana hapa kuhusu Maliasili na Utalii watakapoona jambo hilo na kuangalia assessment pale hali ikoje, nadhani Serikali itafanya maamuzi sahihi kutokana na taratibu zinavyokwenda. Kwa hiyo, hilo naomba Mheshimiwa Oscar aondoe hofu kuhusu ushiriki wa Serikali Kuu katika jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuambatana, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tulikubaliana kuna mambo na changamoto mbalimbali kwamba mara baada ya Bunge la Bajeti tutapanga ratiba maalum kwa ajili ya kufika Biharamulo. Vilevile licha ya changamoto ya pale Nyakanazi, kuna mambo mengine ya msingi uliyazungumza katika siku za nyuma tutakuja kuyajadili pamoja katika Jimbo lako la Biharamulo Magharibi.

Name

Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Primary Question

MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:- Kijiji cha Nyakanazi, Wilaya ya Biharamulo kiko kwenye njia panda kwenda Kigoma, Kahama, Ngara na kina wakazi wapatao 15,000. Kulingana na hali hiyo, kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinaibuka na idadi ya watu inaongezeka kwa kasi; aidha, kijiji hicho pia kimebanwa na hifadhi inayopakana nacho. Je, Serikali ipo tayari kujadiliana na Halmashauri ya Wilaya na wakazi wa Nyakanazi ili kuona uwezekano wa upanuzi wa eneo la kijiji kwa upande wa hifadhi inayopakana na kituo cha polisi kwa nia ya kufungua fursa za kiuchumi?

Supplementary Question 2

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kijiji cha Kasapa wanakabiliwa na changamoto inayofanana na wananchi wa Kijiji cha Nyakanazi. Mwaka huu walikosa kabisa maeneo ya kulima baada ya wahifadhi wa msitu wa TFS Kalambo kuweka mipaka ya eneo lao na kuonekana kijiji na maeneo yote wanayolima, yako ndani ya hifadhi na kwa kuwa Halmashauri tayari imeanza mchakato wa kuliona hilo.
Je, Serikali iko tayari kuungana na mawazo ya Halmashauri pamoja na Ward DC ya Kijiji cha Sintali ili wananchi hawa waweze kupata eneo la kulima?(Makofi)

Name

Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Answer

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na napenda kujibu swali la Mbunge makini sana wa kule Nkasi Kusini, Mheshimiwa Desderius Mipata kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mipata ameleta tatizo hilo tayari kwenye Wizara yetu na nilimuahidi kwamba tutakwenda tuliangalie suala hilo katika site huko na tutafanya maamuzi baada ya hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ahadi yangu iko pale pale na Serikali itatekeleza kama ambavyo itaona inafaa. (Makofi)