Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:- Takwimu zinaonesha upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo zaidi ya 200,000 katika shule mbalimbali za sekondari na msingi. (a) Je, nini mkakati wa Serikali wa kumaliza tatizo hilo? (b) Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuja na mkakati mbadala kama ilivyofanya wakati wa kumaliza tatizo la madawati na maabara nchini?

Supplementary Question 1

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa ruzuku hii iliyotajwa hapa kila Halmashauri imejipangia namna gani itatumia hizo ruzuku na hakuna uniformity katika matumizi hayo, na kama ambavyo tulimaliza suala la upungufu wa madawati na maabara nchini, je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kutoa maagizo makali kidogo ili kumaliza suala hili la upungufu wa vyoo mashuleni?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wanaoteseka sana katika suala zima la upungufu wa vyoo nchini ni hasa mabinti walioko kwenye shule za sekondari. Kila mtu anafahamu wanapokuwa kwenye mzunguko ule kidogo wanapata taabu kulingana na ukosefu wa vyoo tena vyenye maji safi.
Je, ni lini sasa hususani katika Mkoa wetu wa Manyara Serikali itachukua hatua ya kumaliza tatizo hili hasa katika shule ya Komoto na Bagara Sekondari pale Babati Mjini? Ahsante.

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Ester Mahawe kwa swali la msingi pamoja na maswali yake ya nyongeza. Ni changamoto kubwa sana ambayo tunakabiliana nayo na yeye mwenyewe ni shahidi manake ni mdau katika sekta ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyozungumza tumekuwa na mikakati mbalimbali kuhusu miundombinu mbalimbali hususani maabara na madarasa. Lakini kwa wakati huu ambao bado tunahangaika kumalizia ujenzi wa maabara hususani kumalizia maboma ya maabara na kuzipatia vifaa, na bado wananchi wanaendelea kuchangia; mimi nilikuwa namuomba Mheshimiwa Mahawe aungane na sisi kwamba tutoe kwanza kipaumbele kwenye hizi fedha ambazo zimetengwa ili kusudi tuone zitafikia hatua gani wakati huo huo tunamalizia suala la maabara ili baadaye tuweze kuchukua hatua zaidi kama anavyopendekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu miundombinu ya maji katika shule zetu. Tumeshatoa maelekezo kwamba kila shule inapopanga ujenzi wa madarasa ni muhimu sana wakazingatia kuweka miundombinu ya kuvuna maji ya mvua. Hiyo ni miundombinu ambayo ni ya gharama nafuu badala ya kuwa na miradi ya maji ya kutumia vyanzo vingine ambavyo vinatumia fedha nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hilo ni agizo lilishatolewa na maelekezo yalishatolewa. Inatakiwa sasa Wakurugenzi wa halmashauri zote pale ambapo shule inajengwa lazima kuwe na miundombinu ya maji ya mvua, ikiwa ni pamoja na shule ambazo amezitaja, baada tu ya kikao cha leo nitafuatilia kule Halmashauri ya Babati ili kusudi tuweze kujua hizo shule Mkurugenzi ana mpango gani kuzipatia huduma za maji. Ahsante sana.

Name

Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:- Takwimu zinaonesha upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo zaidi ya 200,000 katika shule mbalimbali za sekondari na msingi. (a) Je, nini mkakati wa Serikali wa kumaliza tatizo hilo? (b) Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuja na mkakati mbadala kama ilivyofanya wakati wa kumaliza tatizo la madawati na maabara nchini?

Supplementary Question 2

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa miundombinu hiyo katika vyoo kwenye shule zetu za msingi na sekondari bado haizingatii mahitaji ya watoto wenye ulemavu; na baadhi ya watoto wenye ulemavu wanalazimika kutambaa katika vyoo hivyo ambavyo wakati mwingine ni vichafu na vinahatarisha afya kwa watoto wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nashukuru kwa majibu yake, lakini sijasikia hata yeye mwenyewe kuona kwa jicho la pili uhitaji wa watoto hawa wenye mahitaji maalum katika vyoo hivi. Ni nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kwamba wanazingatia mahitaji ya watoto wenye ulemavu ili na wao waweze kusoma vizuri? Ahsante.

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Amina Mollel kwa kufuatilia hasa hasa masuala yanayowahusu wanafunzi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba michoro ya zamani ilikuwa na upungufu wa kutozingatia mahitaji ya watoto au wanafunzi wenye ulemavu. Hata hivyo michoro ambayo ilipitishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka jana yote imezingatia kwamba darasa, choo na bweni na miundombinu mingine ya shule ambayo inatumiwa na wanafunzi lazima izingatie mahitaji ya watoto wenye ulemavu, na ushahidi ni mabweni mapya na madarasa mapya na vyoo vipya ambavyo vimejengwa tangu mwaka jana mwezi wa saba vyote vimezingatia mahitaji hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Amina Mollel kwenda kufanya ukaguzi kwenye maeneo yote ambayo hatimaye tutaelekeza wafanye marekebisho, ahsante sana.