Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Primary Question

MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:- Serikali iliahidi kutoa shilingi milioni 60 kwa ajili ya mradi wa maji wa Sakare ulioko Tarafa ya Bungu na mpaka sasa imetoa shilingi milioni 20 tu; Je, ni lini fedha iliyobaki itatolewa?

Supplementary Question 1

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Kwanza niipongeze Serikali kwa mpango mzuri wa kunipatia fedha shilingi milioni 18. Nina maswali mawili ya nyongeza. Ukiacha fedha ambayo napewa na Serikali milioni 18 Serikali iliniahidi kunipatia fedha zaidi ya milioni 60 na ikatoa milioni 20 toka 2012 hadi leo hii milioni 40 hawajanipatia. Ni lini ahadi ya Serikali ya milioni 40 ambazo waliniahidi kunipatia ili nimalizie sehemu ya vijiji ambavyo vimebakia vya Kwemshai na Mnungui itatimia?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Shirika Lisilokuwa la Kiserikali liliamua kunipatia fedha na kuchimba visima tisa katika Jimbo langu la Korogwe Vijijini na baadhi ya sehemu Serikali iliamua kuchukua dhamana ya kufunga pampu na kusambaza maji. Katika sehemu hizo Serikali iliamua kwamba katika Kijiji cha Lusanga Mnyuzi, Makuyuni, Kwikwazu pamoja na Kerenge kibaoni kwamba watafunga maji hayo na kuyasambaza. Je, ni lini maji haya yatapelekwa katika vijiji ambavyo Serikali iliamua kwamba watawapelekea maji?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS - TAMISEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na niweke rekodi sawa kwamba milioni 81 si milioni 18 ambayo tumeweka katika mpango wa Serikali wa mwaka huu. Mradi ule kutokana na tathmini tuliyofanya tunahitaji karibuni milioni 415. Kwa hiyo hii sisi watu wa Pwani tunasema kama kiingilia mbago tu. Nakumbuka tulipokuwa na Mheshimiwa Rais pale Korogwe Mheshimiwa Mbunge alizungumza hoja hii hasa ya maji katika jimbo lake na Mheshimiwa Rais aliibeba kwa ukubwa wake katika Wilaya nzima ya korogwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kuwa ni mipango ya Serikali, ukiachana na suala hili la bajeti lakini kwa ahadi ya Mheshimiwa Rais tutafanya kila liwezekanalo ili Wilaya yote ya Korogwe Mjini na Vijijini kama tulivyoelekeza siku ile katika mkutano wetu mambo yatakuwa sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ajenda nyingine ya wafadhili wetu, tunajua kwamba kuna World Vision kule walifanya kazi na taasisi zingine walifanya kazi kubwa sana. Naomba nimhakikishie, Serikali tumeshaanza kutafuta jinsi ya kufanya ili ahadi ya Serikali juu ya maji iwafikie wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jana tulisikia kwenye vyombo vya habari, walikuwa wakionesha jinsi wananchi wa jimbo lake walivyokuwa wakishangilia maji kutokana na juhudi kubwa inayofanywa na Waheshimiwa Wabunge wawili katika Wilaya ya Korogwe. Kwa hiyo niwahakikishie kwamba tutatafuta namna ya kufanya ya pamoja kuzishughulikia changamoto tulizobaini kwa kushirikiana na Wizara ya Maji ili ahadi ya Mheshimiwa Rais iweze kutekelezeka na hivyo wananchi wa Korogwe wapate maji safi na salama.