Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:- Wananchi wa Mji wa Haydom wamekuwa wakiomba Haydom iwe Mamlaka ya Mji Mdogo. Je, ni lini Serikali itaupa Mji wa Haydom hadhi hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, ninayo maswali
mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumeleta maombi haya muda mrefu; na vikao hivi vimekaa muda mrefu; na tuna miji miwili ya Dongobesh na Haydom; na kwa kuwa muda umepita, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa
kutuma wataalamu wake kutoka TAMISEMI ili kushirikiana na wataalamu walioko Wilayani kusaidia vigezo hivi kutimia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri yuko tayari, je, ni lini sasa atawatuma wataalamu hawa ili
kiu ya wananchi wa Mbulu Vijijini itimie?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama
nilivyosema pale, kwanza elekezo langu ni kwamba naomba niwasihi ndugu zetu wa Mbulu kwamba kwa sababu kazi kubwa na Mbunge umekuwa ukipigania jambo hili sana kwa wakati wote kwamba zile taarifa zipite katika vikao vile vya kisheria sasa zije huku kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuwatuma hili jambo, siyo tatizo kubwa sana, kwa sababu hata Mheshimiwa
Flatei kama atakumbuka, kuna team mara ya kwanza ilikuja kule kwa maombi yake vilevile na taarifa tunazo kuhusu Mji huu wa Haydom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Mbunge amesema na suala zima la Mji wa Dogobesh. Kama
nilivyosema mwanzo ni kwamba hata Mji wa Dogobesh wakati unataka upandishwe, lazima taratibu hizi za kisheria ziweze kufuatwa ambapo mamlaka haya kuanzishwa kwake, yanatuletea utaratibu wa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Flatei naomba nikutoe hofu kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, cha kufanya ni kwamba tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo kukupa ushirikiano wote. Ninachokiomba ni kwamba vile vikao vya kisheria viweze kutimiza wajibu wake, tukipata taarifa hizo katika ofisi yetu, nitakupa ushirikiano wote
kuhakikisha Halmashauri yako katika maeneo yako ya Mamlaka Mji Mdogo, basi yaweze kupitiwa na kuweza
kupewa hadhi kama tulivyozungumza.

Name

Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:- Wananchi wa Mji wa Haydom wamekuwa wakiomba Haydom iwe Mamlaka ya Mji Mdogo. Je, ni lini Serikali itaupa Mji wa Haydom hadhi hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa matatizo yaliyoko huko Mbulu yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo Itigi katika Jimbo la Manyoni Magharibi, ni kwamba Itigi ni eneo kubwa sana, lipo katika Wilaya ya Manyoni. Kutoka mwanzo wa Tarafa ya Itigi hadi mwisho kuna zaidi ya kilometa 200 na ni Tarafa moja tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kuuliza swali dogo tu la nyongeza kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuigawa Tarafa hii ya Itigi kuwa Tarafa nyingi kwa sababu ya eneo na jiografia ni eneo kubwa sana?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuko tayari, lakini kwanza lazima mchakato huu uanze katika suala zima la vijiji, itakuja katika vikao vya Ward Council, vitakuja katika vikao vya full council, vitakuja DCC, RCC vitafika kwetu, then Waziri mwenye dhamana, kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura ya 287 kifungu cha 10 ambacho kinafanya variation ya haya maeneo, atachukua jukumu hilo la kufanya hivyo.
Kwa hiyo, ndugu yangu wa Itigi wala usiwe na hofu katika hilo, anzeni mchakato, sisi Serikali tuko kwa ajili ya
kutekeleza hayo ambayo mtayafanya.

Name

Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:- Wananchi wa Mji wa Haydom wamekuwa wakiomba Haydom iwe Mamlaka ya Mji Mdogo. Je, ni lini Serikali itaupa Mji wa Haydom hadhi hiyo?

Supplementary Question 3

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nampongeza ndugu yangu Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya na hasa ya kushughulikia matatizo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika tatizo la kule Mbulu hasa kule Haydom, inalingana kabisa na Korogwe Vijijini
katika Mji Mdogo wa Hale na wewe mwenyewe umeshafika pale; je, Serikali Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Kijiji cha Hale kuwa Mji mdogo kule Korogwe Vijijini?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuliweza kufika pale kwa sababu walikuwa na concern ya Mji wa Mombo. Hayo yote, hata timu yetu tuliituma, waliweza kufika kule na kufanya assessment na wataalamu wameshafanya jukumu lao, iko katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI sasa inafanyiwa kazi. Kwa hiyo, mchakato ukikamilika, basi mtapata mrejesho nini kimepatikana katika eneo hilo.