Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Faida Mohammed Bakar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR (K.n.y. MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH) aliuliza:- Mafuta na gesi ni rasilimali zinazotegemewa kuwa na mchango mkubwa kwa Taifa letu:- Je, ni aina ngapi za gesi zilizogundulika na faida iliyopatikana tangu ugunduzi huo ulivyotokea?

Supplementary Question 1

MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kumrekebisha Mheshimiwa Naibu Waziri kidogo, mimi siyo Mbunge wa Viti Maalum Chakechake. Ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba ikiwemo Chakechake na Mkoani. Ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kama kawaida yake, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania yanaleta uharibifu wa mazingira katika nchi yetu; na kwa kuwa gesi ipo lakini haifikishwi hasa kule vijijini ambako hiyo miti ndiyo inakatwa na kufanywa mikaa: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasambazia wananchi gesi hasa za majumbani kwa ajili ya matumizi na waachane na tabia ya kukata miti na kutengeneza mkaa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa watu wengi wana hamu kubwa sana ya kutumia hii gesi hasa ya majumbani lakini wanaogopa, wanasikia kwamba gesi inaua; hawana elimu hiyo: Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kutoa elimu ya kuwaelimisha wananchi hasa vijijini na mijini ili kuweza kutumia gesi hiyo kwa manufaa ya wananchi wote hasa vijijini na mijini kwa ajili ya matumizi ya kupikia majumbani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Faida kwa jinsi anavyohangaika na kushughulika na kupambana na uharibifu wa mazingira hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ambayo Serikali imechukua katika kuhakikisha kwamba uharibifu wa mazingira unapungua kwa kiasi kikubwa ni kuongezeka kwa matumizi ya gesi asilia hapa nchini. La kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, na hatua ya kwanza ambayo Serikali imeanza, TPDC imeanza sasa mradi wa kusambaza gesi majumbani na katika matumizi ya magari kwa ajili ya Dar es Salaam. Hatua ya kwanza imekamilisha usanifu ambao hivi karibuni utaanza utekelezaji wake na maeneo yatakayoanziwa ni pamoja na maeneo ya Mikocheni, Tabata na Sinza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waharibifu wa kwanza kabisa wa mazingira hapa nchini ni wakazi wa Dar es Salaam. Dar es Salaam na wananchi kwa ujumla ni jumla ya magunia 45,000 yanaingia kwa siku kwa Jiji la Dar es Salaam. Sasa ili kupunguza athari hiyo, hatua ya kwanza ni kupunguza matumizi ya mkaa kwa wananchi wa Dar es Salaam kwa kutekeleza mradi huu.
Awamu ya pili itaenda katika maeneo ya Tabata, maeneo ya Ukonga kwa Mheshimiwa Waitara, lakini maeneo ya Kigamboni na maeneo mengine. Utaratibu huu utaenda sambamba na maeneo ya Lindi na Mtwara ambapo mradi huu pia utaanza mwezi Juni mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo utekelezaji huu wa kutumia gesi utaendelea katika Mikoa ya Morogoro na Dodoma ambayo inakuja kuwa Makao Makuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba matumizi ya gesi yatapunguza kwa kiasi kikubwa sana uharibifu wa mazingira. Huo ni mkakati wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa pili, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imetenga pesa, jumla ya shilingi bilioni 6.5 kwenye bajeti ya mwaka huu ili gesi iweze kusambazwa katika maeneo mengi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu; ni kweli TPDC wameanza kutoa elimu japo siyo kwa kiwango kikubwa. Elimu ya kwanza ambayo imefanyika ni katika maeneo ya minada pamoja na maeneo ya maonyesho, lakini katika Mikoa ya Lindi na Mtwara TPDC imetoa elimu mashuleni, wameanza kutoa makongamano katika maeneo ya Mikoa ya Lindi na Mtwara, Mwanza, Arusha pamoja na Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, harakati za kutoa elimu ili matumizi sahihi yaende sambamba na mahitaji, yanaendelea.

Name

Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Primary Question

MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR (K.n.y. MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH) aliuliza:- Mafuta na gesi ni rasilimali zinazotegemewa kuwa na mchango mkubwa kwa Taifa letu:- Je, ni aina ngapi za gesi zilizogundulika na faida iliyopatikana tangu ugunduzi huo ulivyotokea?

Supplementary Question 2

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Katika Sekta ya Gesi utafiti wa gesi na mafuta katika Bonde la Ziwa Tanganyika pamoja na Chepechepe na Bonde la Mto Malagarasi, tungependa kujua utafiti huo umefikia wapi?

Name

Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Answer

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa majibu mazuri, niongezee lile swali la awali; matumizi ya gesi na mambo ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba sasa hivi Mikocheni na nyumba za TPDC 70 wanatumia gesi, wana mabomba mawili mle ndani; bomba la maji na bomba la gesi. Matumizi yake kwa mwezi hawajavuka sh. 25,000/= hata wakipika vyakula kama maharage, makongoro, ni sh. 25,000. Hiyo tumefanya. Halafu kuna viwanda 37 vinatumia gesi. Hili jana liliongelewa. Tumepata fedha dola milioni 150 kutoka African Development Bank kwa ajili ya kusambaza gesi Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.
Waheshimiwa Wabunge, maana ya uchumi wa gesi ni kwamba hii gesi ni lazima tujenge mabomba mengi. Sasa hivi bomba kubwa la Mtwara – Dar es Salaam liko kwenye asilimia 10 lakini likijaa kabisa gesi, ni mita za ujazo milioni 784 (784 million cubic feet of natural gas) ndiyo inapaswa kupita mle kwa siku. Sasa hivi bado tuko ten percent, lakini ikishafika pale Kinyerezi, ni lazima tujenge mabomba kwenda Morogoro, Dodoma, kila mahali, mpaka Mbeya. Hiyo ndiyo maana ya uchumi wa gesi na ndiyo maana tunasema hii nchi lazima tujenge mabomba mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ya matumizi ni kwamba elimu itakayotolewa Mheshimiwa Mbunge, nadhani siyo muhimu. Gesi ya zamani ndiyo ilikuwa inalipuka, lakini gesi ya kisasa hailipuki. Hii gesi ni CNG (Compressed Natural Gas). Kwa hiyo, ukweli ni kwamba huenda hata elimu haihitajiki, ni kununua unakwenda kutumia tu na ndiyo inaingia kwenye magari. Kwa hiyo, hatuwezi kuweka gesi kwenye gari halafu tena inalipuka. Kituo cha kwanza cha gesi kiko pale Ubungo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye swali lako Mheshimiwa Nsanzugwanko, ni kwamba mkutano wa kwanza, tena nilikuwa sijamweleza Naibu Waziri, naye itabidi aniwakilishe, mzee niwakilishe; kikao cha kwanza kitafanyika Kalemee wiki ijayo cha exploration kwenye Ziwa Tanganyika. Ni kwamba Congo, Tanzania, Burundi na Zambia ni lazima tukae chini; tunajua kwamba kuna gesi na mafuta. Hiyo tunaweza kujua kwa sababu ya ugunduzi kule kaskazini Lake Kivu. Kabla hatujaanza kuzozana, ni afadhali tuanze majadiliano kwamba gesi na mafuta yakipatikana tutakuja kugawana kiasi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, exploration ile tunaifanya pamoja na Mto Malagarasi, tunajua dalili kwamba kuna ama gesi au mafuta, lakini huku gesi tumeshaiona huku Kipili kusini mwa Ziwa Tanganyika huku, ipo. Sasa tunataka kujua ni kiasi gani na ni mafuta kiasi gani.