Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Primary Question

MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:- Kufunguka kwa mawasiliano ya barabara za Tabora, Nzega, Tabora - Manyoni na Tabora - Kigoma kumeleta maendeleo ya kukua kwa Mji wa Tabora na kuongezeka shughuli za uwekezaji na ujenzi wa nyumba za makazi na biashara:- Je, ni lini Serikali italeta Msajili wa Hati za Viwanja Tabora ili aweze kuidhinisha hati za viwanja kwa wakazi na wawekezaji kwa kuwa kwa sasa huduma hizo hazipo Mkoani Tabora?

Supplementary Question 1

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na pongezi zangu kwa niaba ya Wanauyui na Tabora wa ujumla kupeleka Msajili wa Hati, nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa vile kuna upungufu mkubwa sana wa idara mbalimbali za ardhi pale ikiwemo ya upimaji na mipango: Je, Serikali iko tayari kupeleka tena wataalam hao ili wafanye kazi na Msajili huyu wa Hati?
Swali la pili; kwa vile kabla ya kupelekwa Msajili huyu wiki moja iliyopita, kwa miaka mingi iliyopita Hati za Tabora zimekuwa zinasajiliwa katika Ofisi nyingine za Kanda, Dodoma na Mwanza: Je, Serikali sasa iko tayari kurudisha kumbukumbu ya Hati zetu zote pale Tabora? Ahsante sana.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza kuhusu upungufu wa wataalam wa idara nyingine, ametaja mipango miji, kama tuko tayari kupeleka.
Mheshimiwa Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako kwamba kwa sasa katika kipindi hiki ambacho pia tunatakiwa kama Wizara zote au Serikali kuhamia Dodoma, baadhi ya Wataalam ambao wako Makao Makuu tutawasambaza katika kanda ambazo zina upungufu, kwa sababu, maeneo mengi ni karibu yanao wataalam wa kutosha, lakini ni machache likiwepo la Tabora ambao hawana wataalam hao. Kwa hiyo, tutawapeleka katika Kanda ili kuendelea kuziimarisha kama tulivyoahidi.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, amesema Hati zilizoko Mwanza na maeneo mengine ambazo ni za Tabora; naomba nimhakikishie tutafanya utaratibu wa kuhakikisha hati hizo zinarudi katika ofisi husika kwa sababu tayari Msajili ameshapatikana, basi anao wajibu pia wa kuhakikisha anatunza Hati za Maeneo ambayo anayasimamia na yeye wa Kanda ya Tabora ana Mikoa zaidi ya minne.