Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Primary Question

MHE. JUMA H. AWESO aliuliza:- Hospitali ya Wilaya ya Pangani ina uhitaji wa X-Ray ili kutoa huduma hiyo kwa wananchi ambao hutembea mwendo mrefu kufuata huduma hiyo Tanga Mjini:- Je, ni lini Serikali itapeleka X-Ray katika Hospitali hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. JUMA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya kumuuliza. Mimi kama Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Pangani sikubaliani na majibu ya Mheshimiwa Waziri ya kusema kwamba mazungumzo yanaendelea, ilhali wananchi wangu wakitaabika. Tunapozungumzia suala la X-Ray, tunazungumzia uhai wa wananchi wa Jimbo langu la Pangani. Leo wananchi wanatoka Muhungulu, Mkalamo wanafuata huduma ya X-Ray Tanga Mjini.
Sasa nataka nijue ni nini nguvu ya Serikali katika kuhakikisha kwamba inatupatia fedha za dharura ili X-Ray hii ipatikane kwa haraka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, pamoja na changamoto ya ukosefu wa X-Ray bado Hospitali yetu ya Wilaya imekuwa na changamoto lukuki za ukosefu wa dawa pamoja na vifaa tiba. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongozana na mimi baada ya Bunge kuhakikisha kwamba, tunaenda kukabiliana na changamoto ambazo Hospitali yetu ya Wilaya inakabiliana nazo?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lolote haliwezi kukamilika bila ya mazungumzo, ndiyo maana halmashauri pale imefanya utaratibu wa kupata hii milioni 70 kutoka NHIF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba, utaratibu uliowekwa na halmashauri yake na yeye mwenyewe akiwa mjumbe wa Baraza la Madiwani; na nikijua kwamba yeye ni kijana mahiri anapambana sana juu ya suala la afya katika eneo lake; sisi tuta-fast track hiyo process ya kupata X-Ray haraka ili wananchi wa Pangani ambao kwa muda mrefu anawapigania waweze kupata huduma ya afya, lakini nimpongeze sana katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuongozana na Mheshimiwa Mbunge, naomba nimwambie kwamba, niko tayari. Baada ya Bunge, mpango wangu ni kutembelea Mikoa ya Tanga, Lindi, Mtwara, Pwani na Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, tutafika Pangani na tutakagua eneo hilo. Hali kadhalika tutakagua kituo cha afya ambacho wanaendelea kukijenga ili tuone namna ya kukusanya nguvu za pamoja za kuhakikisha kwamba, wananchi wa Wilaya ya Pangani wanapata huduma ya afya.

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JUMA H. AWESO aliuliza:- Hospitali ya Wilaya ya Pangani ina uhitaji wa X-Ray ili kutoa huduma hiyo kwa wananchi ambao hutembea mwendo mrefu kufuata huduma hiyo Tanga Mjini:- Je, ni lini Serikali itapeleka X-Ray katika Hospitali hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa Hospitali yetu ya Manispaa ya Iringa ilifunguliwa ili kupunguza msongamano mkubwa sana uliopo katika Hospitali ya Mkoa, lakini mpaka leo hii Hopsitali hii haina mashine ya X-Ray wala Ultra Sound. Pia hospitali hii imekuwa ikihudumia mpaka wagonjwa wanaotoka Kilolo kwa sababu Kilolo pia Hospitali yao ya Wilaya imekaa vibaya kiasi kwamba wagonjwa wanaotoka kule Kilolo wanakuja kuhudumiwa katika hospitali hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba, kama mashine hizi zingekuwepo zingeweza pia kuingiza pesa ili kuzisaidia ziweze kujiendesha. Je, Serikali sasa inaisaidiaje hospitali hii iweze kupata hizi mashine ili iweze kuhudumia wananchi waliopo katika Manispaa ya Iringa?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nasema ngoja nilichukue hili kwa sababu katika kuangalia kwa haraka haraka sikuweza kufahamu kwamba mpaka hivi vifaa vya X-Ray bado vina changamoto kubwa, lakini naomba tulichukue hili kwa ajili ya kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea kule Kilolo, nilijua kwamba watu wa Kilolo wote wanakuja kupata huduma pale na nilijua kwamba vifaa vyote vimekamilika. Jambo hili tutalifanyia kazi kwa pamoja ili Hospitali hii ya Manispaa iweze kutoa huduma bora kwa wananchi wote kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niseme kwamba tutashirikiana kwa pamoja na Mheshimiwa Ritta Kabati pamoja na Wabunge wengine wa huko ili hospitali ile ambayo ni centre kubwa sana ya magari makubwa yanayopita kutoka nchi za jirani kuja Tanzania iwe na uwezo wa kuwahudumia watu kwa kiwango kikubwa.