Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Primary Question

MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwamilikisha na kutoa Hati za Kimila kwa wananchi wa Nachingwea?

Supplementary Question 1

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa masjala za ardhi ambazo zimejengwa katika Vijiji vya Nakalonji, Mbondo, Namatunu pamoja na Nahimba hizo ambazo zilikuwa zinadhaminiwa na watu wa MKURABITA. Maana ni muda mrefu toka zimeachwa mpaka sasa hivi zinataka kupotea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili nataka nijue, ni nini mantiki ya Serikali kuanzisha Vijiji vya mfano; kwa mfano hivyo vijiji vinne ambavyo nimevitaja ambavyo jukumu hili limeachwa mikononi mwa Halmashauri wakati wanajua Halmashauri zetu hazina uwezo au hazina uchumi wa kutosha kuweza kugharamia kukamilisha hizi hati ambazo mpaka sasa hivi zimesimama na wananchi bado hawajapata?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza alitaka kujua ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa masjala kwa ajili ya kuhifadhia hizo hati miliki za kimila. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kwa sasa Halmashauri inafanya juhudi za kutenga bajeti kila mwaka ili kuweza kukamilisha zoezi hilo. Siyo kujenga tu masjala pia kuna hati 1,170 kama nilivyosema ambazo ziliachwa zilikuwa hazijakamilika kutoka katika hivyo Vijiji vya Mbondo, Nakalonji pamoja na Nahimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pale ambapo watakuwa wametenga fedha ya kutosha kuweza kukamilisha, basi zoezi hili la kujenga masjala na kukamilisha zile hati miliki za kimila ambazo ziliachwa na MKURABITA zitakamilika. Hili ni jukumu pia la Halmashauri wenyewe kuhakikisha kwamba zoezi hili linakwisha, kwa sababu lilikuwa limeshaanza vizuri lakini baadaye likaishia katikati.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anasema nini mantiki ya kuanzishwa vijiji vya mfano katika hili. Mheshimiwa Mbunge labda naomba tu tuelewane kwamba zoezi hili linapofanyika lengo lake kubwa pia ni kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na maeneo ambayo yapo kiusalama zaidi. Usalama wenyewe ni pale ambapo unakuwa tayari umeshapimiwa eneo lako vizuri, unayo hati yako ya kimila ya kumiliki, hapo tayari unakuwa na uhakika wa eneo lile kuwa nalo salama. Taasisi hizi ambazo pengine zilikuwa zikisaidia zilishindwa kukamilisha malengo hayo na kuona kama vile mradi ule haukuwa mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mradi huu ulikumbana na changamoto za ukosefu wa fedha. Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunakuwa na Miji iliyo salama lakini miji ambayo pia imepangika. Kikubwa zaidi ni kumwezesha yule mwananchi kumiliki hati yake ya kimila ambayo itamsaidia, hawezi tu kuwa nayo kama hana pia mahali pa kuhifadhia, haya yote yanakwenda katika utaratibu huo wa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali kuanzisha Vijiji vya mfano ni la msingi na zuri, tunaendelea nalo na ndiyo maana sasa tunazitaka Halmashauri ambazo zilikuwa na huo mradi katika ile miradi ambayo haikwisha, basi waendelee kuweka pesa kidogo kidogo wakamilishe ili kuweza kufikia ile azma ya Serikali ya kuwa na usalama wa milki kwa watu wetu.