Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ng'wasi Damas Kamani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: - Je, Serikali haioni kigezo cha uzoefu katika kuomba kazi ni ubaguzi dhidi ya vijana waliohitimu vyuo wanaolenga kuingia katika soko la ajira?

Supplementary Question 1

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali ya nyongeza;

(i) Je, nini kauli ya Serikali juu ya waajiri wa sekta binafsi ambao bado wanatumia kigezo hiki cha uzoefu kwenye kutangaza ajira?

(ii) Je, Serikali iko tayari kufufua ule utaratibu maalum uliokuwepo mwanzo na kuutengenezea sera ambao utawatambua na kuwapa kipaumbele wahitimu ambao wanajitolea kwenye ofisi mbalimbali za umma kwa ajili ya kupata uzoefu?

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imekuwa inafanya jitihada kubwa hasa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuhakikisha kwamba wale waajiri wanazingatia vigezo ambavyo vinatakiwa katika ukuzaji au uenezaji au ule usimamizi wa soko la ajira. Mojawapo ni katika eneo la watu binafsi ambako nako mara kwa mara tunawaelekeza kwamba lazima vigezo vya kuingia viangaliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwenye sekta binafsi, pamoja na utaratibu ambao sisi kwenye soko la ajira tumeuzoea lakini ni kweli kwamba kwenye sekta binafsi kinachoangaliwa zaidi ni tija ili kuweza kusaidia mtu aweze kupata faida katika jambo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawazo yaliyotolewa na Mheshimiwa Mbunge tunayachukua na tutaendelea kuyasimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo la pili; kwa wale wahitimu ambao wanaomba kazi, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inawatambua; na sasa tuko katika hatua za mwisho, kama nilivyowahi kueleza mwanzo, ya kukamilisha ule muundo mzima au taratibu nzima za jinsi wao pia tunawaingiza katika soko la ajira kwa kuzingatia vigezo. Vigezo hivyo ni pamoja na kigezo cha kuwajengea uwezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa maana ya lugha ya internship, lakini pia, kuweka vigezo vingine ambavyo vitawasaidia vijana waweze kuingia katika soko la ajira kirahisi, nashukuru.