Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stella Simon Fiyao

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Mkoa wa Songwe?

Supplementary Question 1

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, fedha iliyokuwa imetengwa ni shilingi bilioni 6.53 lakini mpaka sasa fedha iliyotolewa ni shilingi bilioni 1.14 hasa ukizingatia sasa hivi tuko mwezi wa Nane wa mwaka wa kibajeti bado miezi minne tu ili tuweze kumaliza mwaka wa fedha. Nataka kujua ni mpango upi wa Serikali kuhakikisha mnapeleka fedha zote kwa wakati ndani ya mwaka huu wa bajeti ili chuo hiki kiweze kujengwa kwa wakati?

Swali langu namba mbili, nataka kujua, je, Serikali mna mkakati gani sasa wa kuhakikisha mnapata wakufunzi wa kutosha na wanafunzi ili chuo hiki kitakapoanza kiweze kufunguliwa kwa muda na kuanza kwa wakati, nashukuru sana. (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stella Fiyao, kama alivyouliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ni kweli kwamba kulikuwa na ucheleweshaji kidogo wa upelekaji wa fedha katika fedha ambayo ilikuwa imetengwa ya shilingi bilioni 6.53 lakini mpaka hatua hii ninavyosema shilingi bilioni 1.14 imekwenda na katika mwaka huu wa fedha katika hatua hii ya mwisho tayari kuna fedha zingine ambazo tunatarajia kuzitoa kwenye disbursements nyingine. Changamoto tu ilikuwa ni ya upatikanaji wa fedha lakini azma ya Serikali na dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassani ya kujenga imeendelea kuwepo na siyo tu kwa Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge atakumbuka kuwa tunajenga eneo la Mbozi katika Halmashauri ile lakini pia kwenye Mikoa mingine ujenzi unaendelea. Kwa hiyo, usiwe na wasiwasi nafurahia kwamba ana dhamira ya dhati kuona kwamba chuo kile kinaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, fedha zitapelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza kama tunao mpango gani kuhusiana na kupeleka wakufunzi pamoja na wanafunzi wa kujifunza pale. Dhamira ya Serikali ya kujenga vyuo hivi katika andiko lake kuu ni pamoja na uwepo wa vitendeakazi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanakuwepo lakini pia vifaa vya kijifunzia na mashine za wanafunzi hawa kujifunza, yote haya yako katika mpango wa bajeti na kwamba tutaenda kukamilisha mara pale chuo kitakapokamilika ili wanafunzi hawa wa Kitanzania waweze kupata fursa hiyo ya kujifunza na kuchangia katika ujenzi wa Taifa, ahsante. (Makofi)