Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:- Je, kwa nini Serikali isitumie teknolojia na vifaa vya kisasa kusafisha barabara za TANROADS?

Supplementary Question 1

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niseme tu nasikitika na majibu kwa sababu nilielekeza swali langu TANROADS kwa maana ya highways, lakini hapo anajibu vikundi vilivyosajiliwa na Halmashauri, Manispaa na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutumia teknolojia ya kisasa kwa maana ya magari yangeweza kuwa yanasafisha hizi highway usiku ambapo kuna msongamono mdogo sana wa magari. Nataka kujua, Serikali imeshafanya cost benefit analysis kuweza kujua matumizi ya vifaa vya kisasa vis a vis wanavyosafisha kwa mikono ina faida gani kwenye uchumi wa Kitaifa? Kwa maana vifaa vya kisasa vinapunguza msongamano wa magari, ajali na madhara mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali imeshafanya tafiti kuweza kujua madhara wanayopata wananchi wanaofanya usafi kwa mikono kusafisha barabara na mitaro? Wameshafanya tafiti za kiafya kujua madhara wanayopata wananchi? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, wazo la Mheshimiwa Mbunge Serikali imelichukua, hilo la kwanza.

Suala la pili, ni kwamba TANROADS pia ina barabara ambazo ziko katika Majiji, Miji, Manispaa na hata katika Halmashauri za Wilaya. Hayo maeneo ndiyo hasa ambayo yameonekana yanakuwa na uchafu mwingi ambayo yanahitaji kufanyiwa usafi. Hata hivyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi ya kufanya usafi wa barabara huwa tunatoa kwa wakandarasi na hawajalazimishwa kwamba ni lazima watumie watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana kwa sasa pale Dar es Salaam tayari tuna wakandarasi wawili ambao wameshaanza kutumia teknolojia hii ya kutumia magari kusafisha barabara zetu. Pia, namkumbusha Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna Sheria inayotutaka katika kila mwaka vikundi vingapi, watu wangapi ambao wamepewa kazi hizi za kufanya usafi, kwa hiyo ni takwa pia la kisheria ambalo ni lazima tulitimize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tutakapokuwa tumejiridhisha, kwamba kuna haja sasa pengine ya kubadilisha sheria kwamba tuelekeze zaidi kwenye matumizi ya vifaa vya kisasa, hilo litafanyika na ndiyo maana tumesema wazo hilo tumelichukua. Hili ni pamoja na kuangalia kama kuna madhara kiasi gani ambayo wanaofanya usafi kwa njia ya mikono ambavyo ni vikundi vya watu maalum hasa vikundi vya akinamama na vijana ambavyo mara nyingi ndiyo vitakuwa vinafanya kazi. Tutafanya hizo tafiti kwa kuwa hilo wazo tumelichukua na tutalifanyia kazi, ahsante.