Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. CHARLES S. KIMEI aliuliza; Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa soko la Kimataifa katika eneo la Lokolova mpakani mwa Tanzania na Kenya?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Je, Mheshimiwa Waziri atakubali kuongozana nami kutembelea eneo hili ili aone umuhimu wake na fursa zilizopo kwa kuongeza ajira na biashara kwenye ukanda huu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki?

Mheshimiwa Spika, la pili; kwa vile Serikali imeanza sasa kuboresha mazingira ya machinga huku mjini kwa kuwajengea maeneo mazuri na kuwawekea mapaa kwenye biashara zao.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwezesha wanawake, akinamama, mabinti zetu kule kwenye vijiji ambao wanaenda kwenye magulio kama yale ya Mwika, Kisambo, Marangu, Lyamombi, Kinyange wakinyeshewa mvua mazao yao yakiharibiwa kwakati mvua zinaponyesha ni pamoja na kupigwa na jua kali. Je, Serikali haioni haina mkakati wa kuwajengea mapaa angalau kwenye maeneo machache kwenye masoko haya? (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Charles Kimei, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Dkt. Kimei kwa ufuatiliaji kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo la Vunjo amekuwa akifuatilia sana kuhusiana na ujenzi wa masoko.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu kuongozana nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Bunge hili tutapanga na tutaongozana ili tuweze kutembelea maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili ni kweli Serikali inapambana kuhakikisha tunaweka miundombinu wezeshi ikiwemo masoko, maeneo ya kuuzia bidhaa mbalimbali hasa kwa wanawake, vijana na wamachinga na hii Serikali imeshaanza kupitia TAMISEMI kujenga mabanda na kuezeka maeneo mbalimbali ambayo yanatumika kama masoko ili kuhifadhi bidhaa wakati wa mvua na jua ili wakinamama wafanyabiashara waweze kufanyakazi. Naomba halmashauri waweze kufanya hivyo ili kuhakikisha bidhaa hizo zinatunzwa na kuuzwa katika mazingira mazuri, nakushukuru.