Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 7 Sitting 19 Home Affairs Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 171 2022-05-10

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -

Je, ni ipi kauli ya Serikali juu ya matukio ya moto katika Masoko kwenye maeneo mbalimbali nchini?

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, alijibu: -

Mheshimiwa Spika; kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwa na matukio ya moto katika baadhi ya masoko nchini. Uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine umebaini sababu mbalimbali za matukio hayo. Sababu hizo ni pamoja na uunganishwaji holela wa mifumo ya umeme, kutokuzingatia tahadhari za moto kwa mama lishe na baba lishe na shughuli za uchomeleaji holela wa vyuma katika masoko.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na vyanzo vya matukio hayo umefanyika ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto sambamba na utoaji wa elimu na mafunzo ya matumizi ya vifaa vya awali vya kuzima moto katika masoko nchini. Aidha, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji inashirikiana na Halmashauri zote kuboresha miundombinu ya kuzima moto katika masoko na kuhakikisha ramani za masoko mapya zinakaguliwa na zinakidhi vigezo vya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusisitiza uwepo wa vifaa vya awali vya uzimaji moto, uwepo wa ulinzi wa masoko kwa saa 24 na kuzingatia utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa maalum za kaguzi zinazotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Nashukuru.