Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 10 Sitting 9 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 134 2023-02-10

Name

Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha za kutosha za ujenzi wa barabara za Wilaya ya Same baada ya kutengewa 9.5% tu ya fedha za TARURA kwa mwaka 2018/2019?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Same ina mtandao wa barabara zipatazo kilometa 874.64 ambazo ni sawa na asilimia 18.89 ya mtandao wote wa barabara katika Mkoa wa Kilimanjaro wenye kilometa 4,629.45.

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2018/2019 Wilaya ya Same ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 1.29 sawa na asilimia 12.81 ya bajeti ya Mkoa wa Kilimanjaro ya shilingi bilioni 10.13. Hata hivyo, bajeti kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara katika Wilaya Same imekuwa ikipanda kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Wilaya ya Same ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 3.70 sawa na asilimia 16.24 ya bajeti ya Mkoa ya shilingi bilioni 22.83. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 5.80 sawa na asilimia 18.32 ya bajeti ya Mkoa ya shilingi bilioni 31.65.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Same kadri ya upatikanaji wa fedha kwa kuzingatia mtandao wa barabara uliopo.