Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 10 Sitting 1 Good Governance Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) 5 2023-01-31

Name

Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Primary Question

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -

Mpango wa TASAF kwa Zanzibar umenufaisha kaya 216, Unguja Shehia 204 na Pemba Shehia 78 ambapo ni sawa na 70% ya Shehia zote Zanzibar.

Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha Shehia zote 388 Zanzibar zinanufaika na mpango wa TASAF kwa 100% badala ya 70%?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chake Chake, kama ifuatavyo: -

Mgeshimiwa Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulipoanza utekelezaji mwaka 2013, rasilimali zilizokuwepo zilitosheleza kufikia asilimia 70 ya Vijiji, Mitaa na Shehia ambavyo kwa hesabu ni maeneo 9,960. Kipindi cha kwanza cha Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa kilidumu kwa miaka sita na kilikamilika mwezi Desemba 2019. Katika awamu hiyo, idadi ya maeneo ambayo hayakufikiwa ni Vijiji, Mitaa na Shehia 5,590 nchini kote zikiwemo Shehia 388 za Zanzibar (Unguja ikiwa ni Shehia 259 na Pemba Shehia 129).

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF kilianza rasmi mwezi Januari, 2020. Sehemu hii ya Pili inatekelezwa katika Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba, kwenye Vijiji, Mitaa na Shehia zote ikiwa ni pamoja na zile ambazo hazikufikiwa wakati wa utekelezaji wa kipindi cha kwanza. Utambuzi na uandikishaji wa walengwa katika maeneo yote 5,590 ambayo hayakufikiwa katika kipindi cha kwanza tayari umeshafanyika.

Mheshimiwa Spika, utambuzi ulitanguliwa na semina za uelimishaji kuhusu TASAF na taratibu zake, vigezo vya walengwa na majukumu ya wadau katika ngazi za jamii, shehia, Halmashauri na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar. Aidha, kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana wakati wa utekelezaji wa kipindi cha kwanza, taratibu za utambuzi wa walengwa zimeboreshwa ili kutambua kaya zinazokidhi vigezo. Aidha, tathmini ya hali ya walengwa waliodumu kwenye Mpango katika kipindi cha kwanza itafanyika kwa lengo la kubaini wale ambao wameshaimarika kiuchumi ili kusitisha utoaji wa ruzuku kwa kaya hizo. Naomba kuwasilisha.