Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 7 Sitting 4 Water and Irrigation Wizara ya Maji 35 2022-04-11

Name

Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji Igando - Kijombe ili kupunguza changamoto ya maji Jimbo la Wanging’ombe?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe ni wastani wa asilimia 76. Katika kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Wanging’ombe, Serikali inatekeleza Mradi wa Maji ya Mtiririko wa Igando – Kijombe ambao utahudumia wakazi wapatao 14,377 katika vijiji 10 vya Malangali, Igando, Mpanga, Luduga, Mayale, Kijombe, Wangamiko, Hanjawanu, Iyayi na Lyadebwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji, chujio, ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilometa 28.9 na mabomba ya usambazaji yenye urefu wa kilometa 18.2; ujenzi wa matenki mawili ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita 150,000 na lita 100,000, vituo vya kuchotea maji 22 na mabirika mawili ya kunyweshea mifugo (cattle trough). Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2022 na kuboresha huduma ya maji kutoka asilimia 76 ya sasa na kufikia asilimia 80.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi iliyoainishwa katika mpango wa kuhakikisha lengo la kufikisha huduma ya maji vijijini ni asilimia 85 na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025.