Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 6 Sitting 13 Works, Transport and Communication Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari 158 2022-02-17

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya udanganyifu mkubwa kwenye mikataba ya Ushuru wa kampuni za Simu na wenye maeneo pale panapojengwa minara ya simu kiasi cha kusababisha ushuru kwenda kwa watu wasiohusika?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeir Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kwa mtumiaji wa mwisho huwezeshwa na minara ambayo kwa kiasi kikubwa hujengwa ardhini, lakini pia husimikwa katika majengo marefu, hususan katika maeneo ya miji mikubwa. Ardhi ambayo hutumika katika ujenzi wa minara humilikiwa na wananchi ama taasisi za umma au taasisi za kijamii ambapo hupangishwa kwa mtoa huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, katika kubaini eneo linalopaswa kujengwa mnara wa mawasiliano vigezo mbalimbali vya kitaalam hutumika kama vile uimara wa ardhi, eneo linalowezesha mnara husika kuwasilisiana na minara mingine na maeneo yanayoweza kufikiwa na mawasiliano kupitia mnara husika. Vigezo hivi na vingine ndio vinaweza kuamua mahali sahihi ambapo mnara unaweza kujengwa. Kwa utaratibu uliopo sana, eneo likibainika kukidhi vigezo vya kitaalam, mtoa huduma hufanya mawasiliano na mmiliki wa eneo husika pamoja na Serikali ya eneo hilo ili eneo hilo liweze kujengwa mnara wa mawasiliano. Mtoa huduma huingia mkataba na mmiliki wa eneo ambapo mmiliki huyo hulipwa fedha ya pango la ardhi kulingana na makubaliano yaliyofikiwa ambayo ndiyo huwekwa katika mkataba.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya minara ya mawasiliano ikiwemo kufuata taratibu katika upangishaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa minara. Vilevile Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umetoa maelekezo katika mikataba wanayoingia na Kampuni za Simu kufuata taratibu zote katika kukodi ardhi ambapo minara hiyo hujengwa kupitia halmashauri husika. Ahsante.