Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 6 Sitting 2 Works, Transport and Communication Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 6 2022-02-02

Name

Kavejuru Eliadory Felix

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Primary Question

MHE. KAVEJURU E. FELIX Aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanua Uwanja wa Ndege wa Kigoma ili Ndege kubwa ziweze kutua?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa idhini yako naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini ili niweze kumsaidia katika nafasi hii naomba nimuahidi yeye Mheshimiwa Rais, Waheshimiwa Wabunge pamoja na watanzania kwa ujumla kwamba nitaendelea kuwatumikia kwa uaminifu na uadilifu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanja cha Ndege cha Kigoma ni miongoni mwa Viwanja vya Ndege vinne (4) ambavyo ni Kigoma, Tabora, Sumbawanga na Shinyanga vinavyotarajiwa kujengwa na kukarabatiwa kwa Ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank -EIB). Ambapo miradi mingine yote imekwishapata Makandarasi isipokuwa mradi wa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma. Kwa sasa, taratibu za makubaliano ya Kimkataba tayari zimeshakamilika kati ya Serikali na Mfadhili huyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma kuwa na Mfadhili, kazi zingine ambazo ziko nje ya makubaliano zitatekelezwa na Serikali moja kwa moja. Aidha, Serikali itahusika na kazi ya urefushaji wa barabara ya kuruka na kutua Ndege kutoka mita 1,800 zilizopo kwa sasa hadi mita 3,100. Ambapo tayari Usanifu wa kina umefanyika kwa lengo la kuwezesha ndege kubwa kutua na kuruka bila matatizo yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kazi zinazofadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank - EIB) katika mradi wa Kiwanja hiki cha Ndege, Serikali inasubiri idhini (no objection) kutoka kwa Mfadhili ili kukamilisha mchakato wa manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi atakayetekeleza mradi huu. Aidha, kazi ambazo zinatarajiwa kufanywa kwa ufadhili wa Benki hiyo ni Ujenzi wa Jengo jipya la Abiria, Jengo la Kuongozea Ndege, Upanuzi wa Maegesho ya Ndege, Usimikaji wa taa za kuongozea ndege pamoja na uzio wa usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali imejipanga kuanza upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma mara baada ya kumpata Mkandarasi atakayetekeleza mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.