Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 6 Sitting 2 Water and Irrigation Wizara ya Maji 4 2022-02-02

Name

Charles Muguta Kajege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Primary Question

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA K.n.y. MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza dhamira yake ya kuwatua Wanawake ndoo kichwani kwa kuwasogezea huduma za maji safi na salama karibu na makazi yao katika Jimbo la Mwibara?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuamini sisi Wizara ya Maji. Nataka niahidi Waheshimiwa Wabunge na watanzania mimi Jumaa Aweso na timu nzima ya Wizara ya Maji, hatutokuwa kikwazo kwa watanzania kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya timu nzima ya Menejimenti ya Wizara ya Maji tunatoa pongezi kwa Mheshimiwa Spika Dkt. Tulia Ackson kwa kuaminiwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sisi Wizara ya Maji tutatoa ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha tunafanikisha Bunge hili letu tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Muguta Kajenge, Mbunge wa Mwibara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la Serikali ni kuhakikisha kuwa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ni ya uhakika na endelevu. Kwa sasa, upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Bunda ambapo Jimbo la Mwibara lipo wastani wa asilimia 69 kupitia visima virefu na vifupi 237 vya pampu za mkono, chemchemi moja na skimu za mtandao wa bomba tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali inaendelea na mpango wa muda mfupi wa kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Mwibara kwa kutekeleza miradi mipya ya Buzimbwe, Bulendabufwe, Igundu, upanuzi wa mradi wa maji Iramba kwenda vijiji vya Mugara, Nyarugoma na Muhura. Kazi zinazofanyika kwa miradi mipya ni pamoja na ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 135,000, ujenzi wa vituo 28 vya kuchotea maji, ujenzi wa ofisi moja ya jumuiya ya watumiaji maji na ujenzi wa nyumba ya mitambo (pump house).

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kazi zinazofanyika kwa mradi wa upanuzi ni pamoja na ulazaji wa mabomba umbali wa Kilometa 18.6, ununuzi na ufungaji wa pampu mpya (surface pump). Miradi hii kwa sasa imefikia wastani wa asilimia 15 za utekelezaji na inatarajia kukamilika mwezi Juni, 2022. Kukamilika kwa miradi hii kutaboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa Wilaya ya Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Bunda inapatiwa ufumbuzi wa kudumu, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 itakamilisha usanifu wa mradi wa maji wa Kisorya kupitia chanzo cha maji cha Ziwa Vicktoria. Mradi huo umepangwa kuhudumia vijiji 12 vya Sunsi, Masahunga, Kisorya, Nambubi, Mwitende, Nansimo, Nambaza, Busambara, Mwibara, Kibara A, Kibara B na Kasahanga. Ujenzi wa mradi unatarajiwa kutekelezwa kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 baada ya usanifu kukamilika. (Makofi)