Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 59 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 490 2021-06-25

Name

Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Primary Question

MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kuzipandisha hadhi barabara za ndani za Jimbo la Kawe ili zihudumiwe na TANROADS kwa kuwa uwezo wa TARURA kuhudumia ni kilometa 120 wakati Jimbo lina barabara zenye jumla ya kilometa 1,463?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la kupandisha hadhi barabara ni la kisheria na huzingatia vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009. Barabara ambayo inakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi inatakiwa ijadiliwe kwenye Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa husika na ikionekana inakidhi vigezo vyote Bodi ya Barabara ya Mkoa husika itamshauri Waziri mwenye dhamana na barabara kuwa barabara husika imekidhi vigezo vya kuwa na hadhi ya barabara ya Mkoa na hivyo ipandishwe daraja na kuwa barabara ya Mkoa chini ya Wakala wa Barabara Tanzania kwa maana TANROADS. Hivyo, ni vema taratibu hizo zikafuatwa ili kupandisha hadhi barabara zilizopo katika Jimbo la Kawe.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuiongezea bajeti TARURA ili kuiwezesha kuzihudumia barabara zake ikiwemo kuongeza tozo kwenye mafuta katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 itakayowezesha TARURA kupata fedha kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara.