Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 52 Health and Social Welfare Wizari wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto 433 2021-06-16

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-

Je, uwepo wa Kiwanda cha kuua mazalia ya Mbu (Tanzania Biotech Product Limited) umesaidia vipi mapambano dhidi ya Malaria nchini?

Name

Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hawapo, inakuwa shida sana kuwaona mpaka uvae miwani ya x-ray. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lilikuwa linauliza je, uwepo wa kiwanda cha kuua mazalia ya mbu kimesaidia vipi mapambano dhidi ya malaria nchini? Tangu Kiwanda cha Tanzania Biotech Product Limited kuanza uzalishaji mnamo mwaka 2016, jumla ya lita 340,520 za viuadudu zimenunuliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 ambazo ni wastani wa shilingi 13,200/= kwa lita. Lita hizi za viuadudu zilisambazwa katika Mikoa 28 na kuzifikia Halmashauri zote 185 nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi hizi ziliungana pamoja na utekelezaji wa afua zingine za udhibiti wa malaria zikiwemo matumizi ya vyandarua, kupulizia viatilifu - ukoko ndani ya nyumba hasa kwenye maeneo yenye kiasi kikubwa cha maambukizi ya malaria na uwepo wa vipimo na dawa zenye ubora kwenye kutibu wagonjwa watakaothibitika kuwa na malaria. Hivyo, matokeo ya juhudi hizi ni kuwa, zimefanikisha kupungua kwa idadi ya Mikoa yenye hatari kubwa ya maambukizi ya malaria kutoka Mikoa 11 mwaka 2017 hadi Mikoa Saba mwaka 2020. Aidha visa vipya vya malaria vimepungua kwa asilimia 35 kutoka wagonjwa 162 kwa kila watu 1000 mwaka 2015 hadi wagonjwa 106 kwa watu 1000 mwaka 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kutumia bidhaa za Kiwanda chetu cha Kibaha kwa ajili ya kuchangia jitihada za Serikali kufikia kumaliza Malaria (elimination) ambapo tumedhamiria kuwa ifikapo 2025 kiwango cha malaria kiwe kimepungua hadi kufikia asilimia 3.5 kutoka asilimia 7.5 ya mwaka 2017. Aidha, Serikali itahakikisha kila Halmashauri inaendelea kuwajibika kwenye kuhakikisha kuwa inatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya utekelezaji na hapa wanafanya vizuri. Mwaka huu wa fedha tunaoenda kuuanza mpya wametenga bilioni 2.7 lakini ilikuwa milioni 600 mwaka 2020/2021. Kwa hiyo tunaenda vizuri. Ahsante.