Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 50 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Waziri wa Mifugo na Uvuvi 412 2021-06-14

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Bandari ya Uvuvi na kununua Meli ya uvuvi katika Mkoa wa Mtwara?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo Mbunge wa Mtwara Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uvuvi ya Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 – 2025 Ibara 43(a) ambazo zimeainisha kujenga Bandari ya Uvuvi katika Ukanda wa Pwani ambayo itawezesha meli zinazovua Bahari Kuu kutia nanga kwa lengo la kushusha samaki na mazao ya uvuvi, kuuza samaki, kutoa takwimu sahihi na huduma nyinginezo ikiwemo kujaza mafuta, vyakula na matengenezo madogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutekeleza Mpango huo, Serikali iliingia mkataba na mshauri elekezi ili kubaini eneo linalofaa kwa ujenzi wa bandari. Baada ya uchambuzi huo, mshauri elekezi alipendekeza bandari ijengwe katika eneo la Mbegani – Bagamoyo, na kazi hiyo itaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na mahitaji na uwepo wa bajeti Serikali itaendelea kutazama uwezekano wa kujenga Bandari za Uvuvi katika maeneo mengine ikiwemo Mkoa wa Mtwara kwa siku za usoni ikiwa ni pamoja na kuboresha mialo, kuimarisha vikundi wa usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi na kuanzisha Vyama Vya Ushirika wa Wavuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji na ujenzi wa Bandari za Uvuvi utawezesha kukua kwa biashara na shughuli za uvuvi Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi ikiwemo Mkoa wa Mtwara.