Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 2 Sitting 2 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 25 2021-02-03

Name

Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Primary Question

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia umeme vijiji 32 vya Jimbo la Lushoto ambavyo havina umeme?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto na tabibu wetu humu ndani, kwa wale ambao tunaamini kikombe, kama ifuatavyo:- (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha. Malengo ya Serikali ni kufikisha umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara ifikapo Desemba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili (REA III round two). Kwa Wilaya ya Lushoto Mradi wa REA III mzunguko wa pili unapeleka umeme katika maeneo ya vijiji vyote 32 vya Jimbo la Lushoto ambavyo havikupata umeme kupitia miradi ya kusambaza umeme ya awamu ya pili na awamu ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za mradi ya kusambaza umeme kwa Wilaya ya Lushoto zinajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33; urefu wa kilomita 131.8; njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 umbali wa kilomita 381.9; ufungaji wa transfoma 99 za 50kVA; pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 1,984. Mradi unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 16.8. Utekelezaji wa mradi utaanza Februari, 2021 na kukamilika ifikapo Desemba, 2022.