Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 32 Foreign Affairs and International Cooperation Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 267 2019-05-21

Name

Mgeni Jadi Kadika

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-

Katika jitihada za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za kuboresha uchumi, viongozi wa Jumuiya hiyo walipitisha utengenezaji wa Bandari ya Wete – Pemba;

Je, mpango huo umefikia wapi?

Name

Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA
MASHARIKI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum napenda kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Bandari ya Wete ni mojawapo ya miradi 17 ya mfano (flagship projects) inayosimamiwa na wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyopitiswa katika mkutano wao wa kazi (retreat) uliofanyika mwezi Februari, 2018 Jijini Kampala, Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi inayotekelezwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ile yenye sura ya kikanda (Mradi uweze kunufaisha nchi zaidi ya moja) ambapo nchi wanachama wamekubaliana kuitekeleza kupitia utaratibu wa kutafutiwa fedha kutoka kwa wabia wa maendeleo na kuitangaza kwa wawekezaji kikanda. Miradi hiyo hutekelezwa kwa kuzingatia mikataba inayoingiwa na nchi wanachama inayowezesha kukopeshwa fedha za utekelezaji. Aidha, ulipaji na gharama za utekelezaji wa miradi hiyo hufanywa na nchi mwanachama inayonufaika moja kwa moja kutokana na mradi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kuendeleza mradi wa Bandari ya Wete upo palepale Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuifanyia matengenezo bandari hiii ili iendelee kutoa huduma nzuri kwa wananchi. Matengenezo ambayo yamekwishafanyika ni pamoja na kutengeneza upana wa gati kufikia mita tisa na urefu wa mita tatu kuelekea baharini, na kulikarabati gati yote yenye urefu wa mita 54. Matengenezo hayo yaligharimu kiasi cha shilingi 473.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar imeshafanya mazungumzo na mwekezaji mzawa katika kuendeleza Bandari ya Wete. Tayari makubaliano ya mwanzo baina ya Wizara husika kupitia Shirika la Bandari Zanzibar na mwekezaji yameshafanyika na hivi sasa mwekezaji kwa kushirikiana na wataalam wa shirika la bandari wamo katika maandalizi ya kufanya upimaji (surveying) ya eneo lililopendekezwa kuwepo bandari ili kutayarisha michoro (usanifu) inayohitajika kuwezesha hatua nyingine za ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha miradi ya kipaumbele iliyopitishwa na wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye maslahi mapana kwa Taifa letu inatekelezwa ikiwa ni pamoja na kufuatilia upatikanaji wa rasilimali fedha.