Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 18 Sitting 5 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 58 2020-02-03

Name

Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Primary Question

MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-

Mkoa wa Mtwara una jumla ya Vijiji 869 na Vitongoji 1,826 na jumla ya Vijiji 372 vimethibitishwa kupatiwa umeme ikijumuishwa kufanya Vijiji vitakavyosalia kuwa 497 na hii ni sawa na wastani wa 23.6% ya utekelezaji wa huduma kwa kila Wilaya ndani ya Mkoa.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutekeleza miradi ya REA katika mkoa huu?

(b) Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Mji wa Masasi ilitengewa Vijiji saba tu kati ya Vijiji 31, je, ni lini vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini katika vijiji vyote vya Tanzania Bara. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2021. Mradi wa REA III Mzunguko wa Kwanza unaoendelea unapeleka umeme katika vijiji 167 vya Mkoa wa Mtwara.

(b) Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Mji wa Masasi mradi wa REA III Mzunguko wa Kwanza unatekelezwa katika vijiji saba ambapo hadi kufika Januari, 2020 vijiji vitatu vya Mumbaka, Mlundelunde na Chanikanguo vimewashiwa umeme. Aidha, mkandarasi anaendelea na kazi za mradi katika Vijiji vya Mayula, Minazini, Mtakuja na Nangose A na B. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivi zitakamilika mwezi Aprili, 2020. Gharama za kupeleka umeme katika Wilaya ya Masasi ni shilingi milioni 658.

Mheshimiwa Spika, vijiji 20 vilivyobaki katika Wilaya ya Masasi vinatarajia kupelekewa umeme kupitia mradi wa REA III Mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza mwezi Februari, 2020. Mradi huu utakamilika mwezi Juni, 2021.