Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 6 Information, Culture, Arts and Sports Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo 50 2019-04-09

Name

Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-

Mkoa wa Manyara, hususani Wilaya ya Mbulu, umewahi kutoa wanariadha mahiri ambao walililetea Taifa heshima kubwa, lakini cha kushangaza wanariadha hao wametelekezwa:-

(a) Je, ni lini Serikali sasa itaandaa utaratibu wa kuwaenzi wanariadha hao?

(b) Je, ni lini sasa Serikali itajenga uwanja kwa ajili ya riadha katika Mkoa wa Manyara ili kuwahamasisha wanariadha wapya?

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, picha anayoichora Mheshimiwa Mbunge ya wanamichezo kutothaminiwa haiendani na hali halisi upande wa wanamichezo nchini waliofanya vizuri na kujituma ipasavyo. Naomba nitoe mifano kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanariadha Filbert Bayi aliyevunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 huko New Zealand mwaka 1974 ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania na mmiliki wa Shule za Filbert Bayi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Suleiman Nyambui, mshindi wa medali ya shaba Mashindano ya All African Games mwaka 1978 na medali ya fedha ya Michezo ya Olimpiki 1980 kwa mbio za mita 5,000 sasa ni Kocha wa Riadha wa Taifa wa Brunei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Juma Ikangaa, mshindi wa kwanza wa mbio ndefu za marathon Jijini New York mwaka 1988 na mshindi wa pili mara tatu mfululizo wa marathon Jijini Boston mwaka 1988 – 1990 ni Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na mratibu wa mashindano ya riadha kwa wanawake (ladies first) yanayodhaminiwa na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA) pamoja na Wizara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Samson Ramadhani, mshindi wa marathon medali ya dhahabu Australia mwaka 2006 ni Afisa wa Jeshi;

Mheshimiwa Mwenyekiti, Gidamis Shahanga, mshindi wa medali ya dhahabu mbio za marathon nchini Canada mwaka 1978, Uholanzi 1984, Nairobi 1988 na Vienna, Austria 1990 ni Mwenyekiti Mstaafu wa Halmashauri ya Katesh Manyara; na wengine wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanamichezo, wakiwepo wanariadha walioliletea Taifa hili sifa na heshima kubwa wanatoka sehemu mbalimbali za Tanzania. Wizara imeanza mchakato wa kuanzisha makumbusho maalum Uwanja wa Taifa ambapo picha za wanamichezo wote walioliletea Taifa letu heshima katika vipindi mbalimbali zitawekwa.