Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 14 Sitting 7 Energy and Minerals Wizara ya Madini 75 2019-02-05

Name

Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y. MHE. AGNESS M. MARWA) aliuliza:-

Wananchi wengi walibomolewa nyumba zao na Mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo, Mkoani Tarime na wengine hawajalipwa fidia ya maeneo yao mpaka sasa. Aidha, Mgodi huo pia umeanza kuchimba chini ya ardhi ya maeneo ya watu (underground mining):-

Je, ni lini Mgodi wa ACACIA uliopo Nyamongo utalipa fidia kwa wananchi hao?

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Agness Mathew Marwa ambalo limeulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Getere, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kusimamia sekta ya madini kwa kuhakikisha uwekezaji unafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi ikiwemo kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo miradi na uendelezaji wa migodi inatake kufanyika na kulazimika kupisha maeneo yao wanalipwa fidia stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi na wanapewa makazi mbadala ambayo yana hali bora kuliko makazi waliyokuwa nayo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uthaminishaji katika maeneo yanayozunguka Mgodi wa North Mara na ulipaji wa fidia umegawanyika katika awamu nyingi kwa kuzingatia vijiji husika kuridhia. Kijiji cha Nyabirama wakazi wake waliothaminiwa wote walilipwa fedha zao isipokuwa wakazi 138 ambao fidia yao iliyoidhinishwa ya shilingi bilioni 3 waliikataa na hundi zao zilitolewa na mgodi na ziko kwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Tarime. Eneo la Kijiji cha Nyabichune lilithaminiwa katika awamu ya 47 lakini wananchi walikataa fidia husika iliyoidhinishwa. Aidha, eneo la Mrwambe lilithaminiwa katika awamu ya 30, 32, 32A na 32B na taarifa yake bado haijaridhiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali. Taarifa hiyo ikisharidhiwa itawasilishwa kwa mwekezaji ili aweze kufidia wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Nyamichele ambacho nacho kina waathirika ambao wanatakiwa kufidiwa kuna changamoto ya uwepo wa taarifa mbili tofauti za uthaminishaji. Katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Mara tumekubaliana ifanyike tathmini mpya katika eneo hilo. Pia uthaminishaji utafanyika katika eneo tengefu la mita 200 (buffer zone 200 meters) lililotengwa kwa ajili ya uhifadhi wa maji ya kemikali na mabaki yanayotokana na shughuli ya uchenjuaji wa madini unaofanyika mgodini hapo. Kazi hii ikikamilika wahusika watalipwa stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la mgodi kubadilisha aina ya uchimbaji kutoka uchimbaji wa wazi (open pit) kwenda kwenye uchimbaji wa chini (underground mining), uamuzi huo ulifanyika baada ya mgodi kufanya utafiti ulioonesha kuwa ilikuwa ni rahisi kutumia njia hiyo badala ya kuendelea na mgodi wa wazi. Niwatoe shaka wananchi wa Tarime kuwa Wizara yangu inafuatilia kwa karibu uchimbaji wa underground unaofanyika hivi leo. Uchimbaji huo unafanyika katika eneo la Gokona kuelekea Nyabigena ndani ya maeneo yao ya zamani ambayo walikuwa wameshachimba toka awali. Hivyo, hakuna eneo ambalo mgodi wa underground unachimba kwenye makazi ya wananchi.