Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 23 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 194 2018-05-07

Name

Kemirembe Rose Julius Lwota

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. KEMIREMBE J. LWOTA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itahakikisha umeme wa uhakika kwenye Kata za Wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishari napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kimirembe Julius Lwota, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nyamagana ina jumla ya Kata 18 ambazo ni Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Rwanhima, Mkuyuni, Mabatini, Luchelele, Igogo, Pamba, Nyamagana, Mirongo, Isamilo, Mbungani, Mahina, Igoma, Butimba, Muhandu na Kishiri. Kata zote hizi zinapata umeme wa Gridi ya Taifa japo baadhi ya maeneo ya Kata hayana umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANESCO inaendelea kujenga miundombinu ya umeme na kusambaza umeme katika maeneo yote ya nchi yetu. Katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Shirika la Umeme (TANESCO) limetenga jumla ya shilingi bilioni nane na milioni mia saba thelathini kwa ajili ya kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu ya umeme ya Mkoa wa Mwanza ikiwepo Wilaya ya Nyamagana na Kata zake ili kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika. Hadi kufikia mwezi Machi, 2018 jumla ya nguzo 519 za umeme wa kati wenye msongo wa kilovoti 11 na 33 na nguzo 188 za msongo wa voti 400 katika Kata za Nyamagana na maeneo mengine ya jiji la Mwanza vimebadilishwa, pia vikombe 807 vilikuwa vimevunjika vimebadilishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha kilometa 33 za msongo wa kati na madogo zimesafishwa kwa kukata miti pamoja na kubalisha waya kwa kilometa 22 zilizokuwa zimechakaa. Zoezi hili la ukarabati linaendelea ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho hayo yamewezesha kuimarika kwa upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Mwanza ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Aidha, kukamilka kwa mradi mkubwa wa kusafirisha umeme wa msongo kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga kumechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa umeme katika Mkoa wa Mwanza. Zoezi la ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya umeme ni endelevu na kiasi cha fedha shilingi bilioni nne kimependekeza katika bajeti ya mwaka huu 2018/2019 kwa ajili kuboresha miundombinu ya umeme ya uhakika Jijini Mwanza.